KAMATI YA MIUNDOMBINU YAAGIZA ICoT IONGEZEWE FEDHA
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Miundombinu, Mheshimiwa Seleman Kakoso ,akizungumza na Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia
ya Ujenzi (ICoT),Mhandisi
Mahmoud Chamle, wakati Kamati hiyo ilipotembelea
na kukagua miundombinu na vifaa vya kufundishia
vya Taasisi hiyo, mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Miundombinu Mheshimiwa Selemani Kakoso, ameitaka Wizara ya Ujenzi na
Uchukuzi kutenga fedha za kutosha ili kuiwezesha Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi
(ICoT) kuwa na miundombinu na wakufunzi wa uhakika na hivyo kuongeza idadi ya
mafundi mchundo na sanifu hapa nchini.
Amesema uwepo wa wataalam hao utaongeza
ufanisi katika miradi ya ujenzi na hivyo kutekeleza kikamilifu dhana ya nchi ya
viwanda kwa kuwa na wataalam wengi wa ndani katoka miradi mingi ya ujenzi.
Akizungumza mara baada ya kukagua Taasisi hiyo
mkoani Morogoro, Mheshimiwa Kakoso amesema ili Taifa lifikie malengo ni vema
likawekeza katika kutayarisha wataalam wengi wa kada za ufundi ili miradi
mikubwa inayojengwa isimamiwe na wataalam wazalendo.
“Tuna miradi mingi ambayo inatekelezwa na Serikali
na inatolewa fedha nyingi ila wanaokwenda kunufaika zaidi ni watu ambao wana
level hiyo ya utaalamu wakati na wengi wanatoka nje ya nchi, hivyo kuna umuhimu
sasa wa kuwaandaa watalamu wetu wengi zaidi”, amefafanua Mwenyekiti huyo.
Aidha, ameiagiza Serikali kupitia Wizara kuongeza
vifaa ambavyo vitawasaidia kuleta utaalamu sambamba na ukarabatiwa miundombinu wezeshi
kwa wanafunzi na wakufunzi wataopata fursa ya
kupata elimu katika taasisi hiyo.
Awali akitoa taarifa ya Taasisi hiyo, Waziri
wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, amesema Wizara
imeunganisha kilichokuwa Chuo cha Ujenzi - Morogoro (MWTI) na Chuo cha Teknolojia
Stahiki ya Nguvu Kazi (ATTI) - Mbeya ili kuwa na Taasisi moja imara ya Mafunzo
ya Ufundi (ICoT) itakayokuwa kituo cha umahiri katika kozi za ujenzi, umeme na
mitambo na hivyo kuwezesha Taifa kuwa na wataalam wengi na mahiri wa kada za
chini na za kati za ufundi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu anayeshughulikia Sekta
ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara
itaboresha bajeti ya taasisi hiyo ya ICoT na kuongeza wakufunzi mahiri ili
kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Akizungumza
mbele ya wajumbe wa Kamati, Mkuu wa Taasisi hiyo Mhandisi Mahamoud
Chamle, amesema jumla ya watumishi 109 wanahitajika ili kuiwezesha taasisi hiyo
kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Katika hatua nyingine Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Miundombinu imekagua karakana ya kutengeneza vichwa vya treni na reli
ya kisasa SGR sehemu ya Morogoro-Dar es salam na kuelezea kuridhishwa na hatua
za ujenzi.
"Tumeridhishwa kwa kazi nzuri inayofanywa
katika wizara hii inatia moyo", amesisitiza Mwenyekiti.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu iko
katika ziara ya kukagua miradi ya ujenzi katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na
Dar es Salaam.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment