KAMATI YA AMANI SHINYANGA YASAINI KITABU CHA MAOMBOLEZO
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga Shekhe
Khamisi Balulisa akisaini kitabu cha Maombolezo ya aliyekuwa Rais wa Tanzania
Marehemu Joseph Pombe Magufuli jana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Na Mwandishi wetu Shinyanga.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa
Shinyanga Shekhe Khamisi Balilusa amesema taarifa za kifo cha
aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania marehemu Dkt. John Pombe
Magufuli zimeliweka Taifa katika mfadhaiko mkubwa kwa kuwa aliwafanya
watanzania waishi katika malengo na makusudio ya mwenyezi Mungu.
Shekhe Balulisa alisema hayo jana alipofika kwenye
Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kusaini kitabu cha maombolezo
ya kifo cha Hayati Rais John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi
mwaka huu.
Shekhe Balilusa alisema kuwa utendaji kazi wa
aliyekuwa Rais Magufuli uliwafanya watanzania waishi maisha ya makusudio ya
Mwenyezi Mungu ya kujipatia kipato kutokana na kufanya kazi kwa kuwa Mungu
hakumuumba mwanadamu kuishi bure bali ni kwa kufanya kazi kwa ajili ya
kujipatia vipato vya halali.
Aidha Shekhe Balulisa aliongeza kuwa Rais Magufuli
aliwafanya watanzania wajitambue na kila mmoja wao kujua nafasi yake na
anawajibika na jambo gani ndio maana kifo chake kimewasononesha sana
lakini kwa kuwa ni utashi wa Mwenyezi Mungu hawana budi kulipokea jambo hilo.
Naye Askofu Raphael Machimu wa Kanisa la EAGT Tanzania
amesema kuwa Msiba huu umekuwa mkubwa kutokana na mambo ambayo Rais Magufuli
amekuwa akiyafanya ambayo yamekuwa faraja kubwa hasa kwa watanzania wanyonge
lakini kazi ambazo amekuwa akizifanya hakuna eneo ambalo halikuguswa na
utendaji wake.
Askofu Machimu aliongeza kuwa Rais Magufuli
atakumbukwa kwa yote aliyoyatenda na ameacha alama kubwa na kuongeza kuwa
makanisani kote watu wanamuombea ili Taifa libaki katika utulivu wake kwa kuwa
ni mshtuko mkubwa umetokea.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela
ameviambia vyombo vya habari mkoani Shinyanga kuwa Serikali Mkoani Shinyanga
imetenga eneo maalum kwa ajili ya wananchi wote mkoani Shinyanga kufika na
kusaini kitabu cha maombelezo ya Hayati Rais Joseph Pombe Magufuli na kwamba
kitabu hicho kitakuwepo kwa kipindi chote cha maombolezo hayo.
Bw. Msovela ametoa wito kwa wananchi wote mkoani
Shinyanga kufika Ofisi za Mkuu wa Mkoa ili kusaini kitabu cha Maombolezo kwa
kipindi hiki kigumu kwa kuungana na watanzania wengine ambao watakuwa wanafanya
hivyo katika maeneo mengine kote Nchini.
Kamati ya Amani ya Mkoa wa Shinyanga pamoja na kusaini Kitabu cha Maombolezo lakini pia walitoa dua zao kuliombea Taifa katika kipindi hiki kigumu lakini pia kumuombea Marehemu Rais Joseph Pombe Magufuli ili apokelewe kwa amani Mbunguni.

Post a Comment