CHOZI LA BINTI KIMITI KWA JPM TOKA UGHAIBUNI


  

KIFO hakizoeleki ingawa kipo na tunaishi nacho, kila uchwao kimekuwa kikichukua wazazi wetu, watoto wetu, dada, kaka, jamaa, rafiki na hata jirani zetu.

Kama kifo kingeweza kuonekana, naamini hakuna mtu angekubali kukutana nacho. Hata walemavu wa miguu wangekikimbia.

Kifo ni fumbo la imani ambalo halijapata wa kulifumbua tangu dunia iumbwe.

Ugumu wa kukiona kifo umekuwa mtihani hata kwa majemedari na mashujaa wa kijeshi. Ushujaa wao unakuwa ni udhaifu mbele ya kifo.

Ubaya wa kifo ni kutokuchagua, kifo kinachukua wema na wabaya, wakubwa na hata wadogo.

Kifo sasa kinailiza dunia, kifo kimemchukua shujaa wa Tanzania, mpambanaji na jemedari wa kweli Dk. John Pombe Magufuli. 

Dk. Magufuli sasa ni hayati, mwili wake umo ndani ya jeneza, amelala, amelala milele na hawezi kupumua tena.

Kwa sasa kaburi ndio makazi yake, hawezi kusimama tena na kuwakemea mafisadi na wadhalimu waliokuwa wakipoka haki za wanyonge.

Mwangi wa vilio vya Watanzania, Waafrika na dunia kwa ujumla, unaelekea kwenye jeneza lake.

Watu wanalia, wanamkumbuka, hakuna anayeamini kama mwamba umeanguka.

Kifo kimetuondolea mpigania haki, kifo kimetupokonya jasiri wa karne ya 21, hakika Dk. Magufuli anastahili kuliliwa milele.

Mimi Prudencia Paul Kimiti ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Uhalifu wa Ushuru wa Forodha ndani ya  Mamlaka ya Mapato na Kodi nchini Uingereza (HMRC), sitaacha kumlilia.

Na ili kutimiza ahadi yangu hiyo nimeiona haja ya kutuma Waraka wangu kwa Watanzania wenzangu.

Imani yangu ni kuwa Waraka wangu huu utasalia kuwa kumbukumbu ya maombolezo yangu kwa Hayati Dk. Magufuli na Tanzania kwa ujumla.

 

*POLE*

 

Nianze kwa kuwashukuru  Watanzania kwa mapenzi mkubwa waliyoyaonesha kwa nchi na kwa Hayati Dk  Magufuli.

Wamemuenzi kishujaa na kuionesha dunia kuwa walikuwa na mapenzi ya kweli ya Dk. Magufuli ambaye alipachikwa majina mengi ya kishujaa kama vile Bulldozer, Jembe na Jiwe.

Pili nachukua nafasi hii adimu  na adhimu kumpa pole Rais Samia Suluhu Hassan.

Wote tunakubali kuwa kwa sasa tumo ndani ya  kipindi kigumu kilichojaa  majonzi na maombolezo makubwa.

Aidha nampa  pole Mama Janeth Magufuli na familia yote ya hayati Dk. Magufuli, ndugu, jamaa, marafiki na kwa Watanzania wote popote walipo duniani.

Kifo cha Dk. Magufuli kimetuumiza wote, na tunapaswa kumwomba  Mwenyezi Mungu azidishe Upendo kwa Watanzania na hasa kwa  mama yetu Rais Samia.

Tunamwomba awe jasiri na shupavu katika kuendelea kuwapigania raia wake hasa wanyonge, kulinda uhuru wetu, maslahi, haki na heshima yetu kama Taifa.

 

Tuna imani kubwa kwamba chini ya uongozi wako imara na shupavu hatuwezi kuwa wapweke wala wakiwa.

Imani hiyo hiyo inatupa matumaini kuwa  utaendelea kutimiza majukumu ya kuliongoza na kulivusha taifa letu kwenye mambo yote yanayolikabili sasa na siku zijazo,  kwenye raha na karaha. 

Tunamuomba Mwenyezi Mungu akulinde, udumu na kuendelea kulinda maslahi ya Watanzania ambayo hayati Dk. Magufuli aliwapigania  siku hadi siku.

Sisi tulio ughaibuni, mioyo yetu inaungana nanyi nyumbani katika maombi,  machumgu, maumivu na huzuni. 

Mola Atupe faraja, subira na utulivu.

 

*RAI YANGU*

 

Rai yangu kwenu viongozi, nawasihi kamwe msiache kuiga na kuyatafsiri maisha ya hayati Dk. Magufuli.

Muenzini  kwa vitendo kwa  kuendeleza yote aliyoyasimamia, kuukataa uzembe, kuikataa rushwa, kuupinga ufisadi na kuwatetea wanyonge na kuipenda nchi yetu kwa kuitakia mema. 

Naamini hakuna linaloshindikana, kama yeye aliweza basi nanyi mnaweza, mnaweza kwa sababu mliyaweza hayo pamoja nae. Yaendelezeni.

 

*MAMA SAMIA ANAWEZA*

 

Mama Samia ni kati ya kinamama jasiri  wanaoweza kuifikisha nchi mahali alipotarajia Hayati Magufuli.

Uzoefu wa kazi aliuonyesha akiwa Serikalini  Zanzibar unatosha kuwa na imani nae. 

Alipoteuliwa na Wabunge wa Bunge la Katiba kumsaidia Marehemu Samuel Sitta, ilidhihirisha wazi kuwa ni mwanamke shupavu na hodari.

Kuwa kwake Makamu wa Rais wa shujaa na sauti ya wanyonge Hayati  Dk. Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano na miezi minne kulitosha kunoa makali yake ya kiuongozi.

Naamini ni Rais mwenyewe kumuamini  Mungu kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake.

 

Mama huyu  anafaa kuendeleza mapambano katika kipindi kingine cha pili.

Mama Samia ni mpambanaji anajua mbinu zote za kivita kwenye mapambano haya ya kiuchumi.

Ni nahodha mwenye uwezo wa kulifikisha salama jahazi hili la Tanzania.

Sisi watanzania bila kujali tupo eneo gani la nchi hii tupo naye na  tutamtakia kheri ili alifikishe jahazi hili salama. 

Poleni Watanzania wenzangu, poleni Waafrika na pole kwa dunia.

Sote tunakiri kuwa kifo hakina huruma na ndio maana imetuchukulia shujaa wetu Dk. John Joseph Magufuli.

Mungu ailaze roho ya mpendwa wetu Hayati Dk. John Magufuli mahali pema peponi. Amen.

 Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

 

No comments