BASHUNGWA KUCHUKUA HATUA KWA MAMENEJA WAZEMBE TEMESA, ATAKA MAJINA KUBAINISHWA
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akisisitiza jambo kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala (hayupo pichani), kuhusu huduma zinazotolewa TEMESA, jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Innocent
Bashungwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro
Kilahala kuwasilisha majina ya Mameneja wa Kanda na Mikoa wa TEMESA ambao wameshindwa
kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi ili waweze kuchukuliwa hatua.
Bashungwa ametoa agizo hilo Aprili 22, 2024 jijini Dodoma kufuatia kupokea malalamiko mara kwa mara kuhusu huduma zinazotolewa na TEMESA ikwemo huduma ya Kivuko cha MV.Tanga Mkoani Tanga ambapo amemuagiza Katibu Mkuu kuingilia kati kubaini changamoto zinazokwamisha kivuko hicho.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala akisikiliza kwa makini maelekezo ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (hayupo pichani), alipohoji utoaji wa huduma za vivuko nchini.
“Mambo mengi ya kiutendaji
yanaletwa kwa Waziri na Katibu Mkuu wakati Watendaji mpo na tumewaamini
kusimamia Taasisi zenu, hasa jambo hili lipo TEMESA. Mtendaji Mkuu kama kuna
mapungufu ya wasaidizi wako bora uje kwa Katibu Mkuu useme huyu atufahi aondoke
kuliko kukaa nao maana hatimaye litakuangukia wewe”, amesema Bashungwa.
Bashungwa amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi Mhandisi Aisha Amour kuangalia namna bora ya usimamizi wa TEMESA katika huduma ya vivuko nchini ili kuleta manufaa na uboreshaji wa huduma za usafiri na usafirishaji ziimarike.
Muonekano wa Kivuko cha MV Tanga ambacho kina uwezo wa kubeba abiria 100, magari 6 sawa na tani 50.
Aidha, Bashungwa ameeleza
kuwa bado TEMESA inaendelea kuwa na mikwamo na kutotekeleza majukumu yake kwa uharaka
pindi tatizo linapogundulika katika Vivuko na hivyo kupelekea kuzorota kwa
huduma hiyo katika baadhi ya maeneo.
“Changamoto ya marekebisho
ya kivuko cha MV Tanga yanaendelea zaidi ya siku 10 sasa lakini leo naulizia
vifaa bado havijafika, kama ‘parts’ ziko Dar es Salaam inachukua masaa mangapi
hadi kufika Tanga? na sio Tanga pekee yake ni maeneo yenye vivuko”, Bashungwa
akimuhoji Mtendaji Mkuu wa TEMESA.
Kwa upande wake, Mtendaji
Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo katika
Kivuko cha MV. Tanga na timu ya wataalam inaendelea na marekebisho ya Kivuko
hicho ili kuboresha huduma zake.

Post a Comment