TATIZO LA MAJI KITONGOJI CHA COAST JUU KATA YA MAGAMBA LINAENDA KUWA HISTORIA

 

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2024 Kitaifa, Ndg. Godfrey Mnzava amewahakikishia wananchi wa Kitongoji cha Magamba Coast Juu Kata ya Magamba, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga tatizo la maji kwenye kitongoji hicho linaenda kuwa historia.

Ameyasema hayo juzi wakati Mwenge wa Uhuru 2024 ulipotembelea na kukagua Mradi wa Maji wa Magamba unaoenda kunufaisha zaidi ya Wananchi 30,000 wa Mji wa Lushoto na viunga vyake.

Akiwa kwenye Mradi huo katika Eneo la Coast, Kata ya Magamba, Mnzava alisema kwamba amepata malalamiko kwamba kuna wananchi wametengwa na mradi huo licha ya kuwa unapita kwenye eneo lao ambapo alitaka ufafanuzi kutoka Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) juu ya ukweli wa Jambo hilo.

Baada ya ufafanuzi wa RUWASA, Ndg. Mnzava alifanya mawasiliano kwa njia ya simu na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso huku wananchi wakisikiliza ambapo Waziri huyo ametoa maelekezo kwa watumishi wa sekta ya Maji Mkoa wa Tanga kufanyia kazi suala hilo.

“Waziri, wananchi wa Kitongoji cha Magamba Coast Juu wameona hawapo kwenye coverage ya mradi huu wakati wameona Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya mradi huu, Mama ametoa bilioni 1.8, lakini wao wanaelezwa hawamo kwenye utekelezaji wa mradi huu, sasa unawaeleza nini kwenye hili?" Alihoji Mnzava.

Akitolea ufafanuzi swala hilo, Waziri Aweso alisema tayari ameshatoa maagizo kwa viongozi akiwemo Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga, Mhandisi Upendo Lugongo kwamba hadi kufikia Aprili 22, mwaka huu Mkandarasi ataejenga Mradi wa Maji wa Coast Juu wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 300 awe amefika kuanza kazi.

Baada ya kuzungumza na Waziri Aweso, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa alielezwa kuridhishwa kwake na ukaguzi alioufanya katika Mradi Mkubwa wa RUWASA ambao utagharimu zaidi ya Bilioni 1.8 ukiwa unatekelezwa na Mkandarasi  M/S PNR Services Ltd wa Dar es Salaam.

No comments