RC RUVUMA ALIVYOWAFARIJI YATIMA 74 CHIPOLE

 

Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas akiwa na Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Rehema Madenge walipotembelea kituo cha kulelea watoto yatima cha Chipole Songea ambapo walitoa msaada wa vitu vyenye thamani ya zaidi ya shilingi laki nane na pesa taslimu shilingi 690,000.

Na Albano Midelo,Songea 

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abass Ahmed ametoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya Zaidi ya shilingi laki nane na fedha taslimu shilingi 690,000 kwa kituo cha Watoto yatima Chipole wilayani Songea.

Kituo hicho chenye Watoto yatima 74 kinamilikiwa na watawa wa Shirika la Mtakatifu Agnes Jimbo Kuu katoliki la Songea.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Abbas amevitaja vitu walivyopewa Watoto hao kuwa ni   mchele kilo 100,maharage kilo 50,mafuta ya kupikia lita 20,sukari kilo 50,unga wa mahindi kilo 50 na sabuni ya unga mifuko miwili.

“Mimi binafsi  nimekuwa na utamaduni katika maisha yangu,nikipata fursa huwa natembelea vituo vya kulelea Watoto yatima, kwa lengo la kuwashika mkono na kuwafariji huwa nafarijika ninapofanya jambo hili ’’,alisema RC Abbas.

Picha ya pamoja Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed akiwa na watoto yatima 74 wa kituo cha Chipole Songea 

Amewapongeza watawa hao kwa upendo mkubwa walionao kwa kuchukua jukumu la kuwahudumia Watoto yatima ambapo amesema jukumu hilo ni la kimungu Zaidi.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Rehema Madenge  amewapongeza watawa hao kwa kwa kuwalea Watoto yatima 74  ambao amesema wanalelewa katika mikono salama kutokana na kituo hicho kuwa kimbilio la Watoto wengi.

Amesema kituo hicho kinaisaidia serikali kulea Watoto yatima na kwamba hakuna malipo yanayostahili kwa kazi hiyo Zaidi ya kuwaombea thawabu kwa mwenyezi Mungu.

Afisa  Ustawi Mkoa wa Ruvuma  Vikta Nyenza  akitoa taarifa ya vituo vya kulelea yatima amesema katika Mkoa mzima kuna Watoto yatima  279 kati yao watoto 74 wanalelewa katika kituo cha Chipole.

Jumuiya ya watawa wa Chipole imemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa msaada wa vitu na fedha na kuwafariji na kuwatia moyo wa kuendelea kuwa na huruma na upendo wa kuwahudumia Watoto yatima.

No comments