Marekani na EU kuiwekea vikwazo vipya Iran baada ya shambulio

 

Marekani na Umoja wa Ulaya wanasema wanatazamia kuiwekea Iran vikwazo zaidi, baada ya mashambulizi yake dhidi ya Israel mwishoni mwa juma.

Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen alisema anatazamia kuchukua hatua "katika siku zijazo", huku mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell akisema umoja huo unalifanyia kazi.

Israel imewataka washirika wake kuwekea vikwazo dhidi ya mpango wa makombora wa Tehran.

Vikwazo vya Umoja wa Mataifa kuhusu mpango huo vilikwisha muda wake Oktoba.

Vikwazo hivyo vilihusishwa na mapatano mapana zaidi ya kupunguza mpango wa nyuklia wa Iran.

Hata hivyo nchi kadhaa zikiwemo Marekani, EU na Uingereza zilidumisha vikwazo na kuongeza vingine vipya.

Mkuu wa majeshi ya Israel, Lt Jenerali Herzi Halevi, alisema siku ya Jumatatu kuwa shambulio la Iran halitapita bila kujibiwa.

Shambulio la kwanza la moja kwa moja la Iran dhidi ya Israel siku ya Jumamosi lilishuhudia wimbi la zaidi ya makombora 300 na ndege zisizo na rubani kurushwa kutoka Iran, Iraq, Syria na Yemen, huku nyingi zikiangushwa na Israel na washirika wake.

Tehran ilisema shambulio hilo lilikuwa la kulipiza kisasi shambulizi linalodhaniwa kuwa la anga la Israel dhidi ya ubalozi wake mdogo nchini Syria tarehe 1 Aprili, ambapo watu 13 waliuawa.

bbc

No comments