UKWELI HUU HAPA. MATUMIZI FEDHA ZA BAJETI 2024/2025. PUUZENI UPOTOSHAJI

 

WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, ametoa ufafanuzi dhidi ya upotoshaji uliofanywa na baadhi ya vyombo vya habari nchini kuhusu vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2024/2025 kwamba vimejikita katika kugharamia mashindano ya AFCON na kulipa madeni.

Dk. Mwigulu amelazimika kutoa ufafanuzi huo leo jijini Dodoma wakati wa uwekaji jiwe la msingi kwenye Jengo la Taaluma la Chuo cha Uhasibu IAA Kampasi ya Dodoma.

“Jana, tumesoma Mpango Maendeleo na Ukomo wa Bajeti ya Serikali. Nikaona chombo kimoja kimeandika ni bajeti ya madeni, uchaguzi na AFCON, yaani kwa upeo wake yule mchambuzi yeye aliona bajeti ya sh. trilioni 49 ni ya mambo hayo tu.

“Sasa Watanzania AFCON bajeti yake ni sh. bilioni 200, kwenye trilioni hizo yeye ameona ni AFCON. Uchaguzi ni sh. bilioni 600 kwa mwaka unaofuata, mwaka huu ni sh. bilioni 300 fedha inayoenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa,” anaeleza Dk. Mwigulu.

Waziri huyo wa fedha alifungukwa kwamba kwenye sh. trilioni 49 ya bajeti ya mwaka 2024/2025 fedha ya uchaguzi ambayo takwa la kikatiba na siyo maamuzi ya Rais au Waziri wa Fedha ni sh. bilioni 300.


FEDHA ZA MAENDELEO

Alibainisha kuwa fedha za maendeleo ni sh. trilioni 16 ambazo wapotoshaji hawajazielezea kwamba zitatumika katika kilimo cha umwagiliaji, elimu ya msingi na juu, mifugo, barabara, umeme vijijini, maji, afya, reli na ukamilishaji Bwawa la Mwalimu Nyerere.

“Yule hakuziona hizo fedha, kaona tuu sh. bilioni 200 za AFCON, kaona sh. bilioni 300 za uchaguzi, kaona madeni,” anasisitiza.

Dk. Mwigulu anasema deni halisi katika bajeti hiyo ya sh trilioni 49 ni sh. trilioni tano ambapo ukiweka riba haizidi sh. trilioni 10.

“Deni lenyewe tunajenga reli, tunajenga vivuko kikiwemo Busisi, vyuo vikuu, mabweni ili watoto wakae sehemu salama, yeye hajaona anaona ni bajeti ya madeni.

“Kaona AFCON sh. bilioni 200, kaona uchaguzi ambao ni jambo la katiba, yeye kaona jambo la ajabu kaandika hivyo, hata AFCON Tanzania kupewa wenyeji ni heshima kwetu kwa sababu kuna nchi hazijapata nafasi hiyo, sisi PR ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imetosha kuwa wenyeji,” alisema.

No comments