Mbowe: Wabunge wamejiongezea mishahara
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe akiongea na wananchi waliojitokeza katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Babati mkoani Manyara jana March 21-2024.
Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa Freeman Mbowe amedai kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamejiongezea mishahara yao kutoka milioni 16 waliyokuwa wanapata hapo awali hadi kufikia milioni 18 kwa mwezi, hiyo ikiwa ni nje ya posho ya vikao anayopatiwa Mbunge kila anapohudhuria kikao kimoja cha Bunge
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Machi 21.2024 Babati mjini, mkoani Manyara Mbowe amesema kuwa mara nyingi viongozi wa serikali wamekuwa wakijitokeza hadharani na kueleza kuwa uchumi umekua hapa nchini, jambo ambalo anakubaliananalo kwa kutumia kipimo cha pato la Taifa (GDP) lakini ameeleza kuwa uchumi huo umekua kwa watu wachache walioko serikalini na sio kwa mtu mmoja mmoja au jamii kwa ujumla wake
Amesema viongozi walioko serikalini wamekuwa wakiendekeza maisha ya anasa ambayo kwa kiasi kikubwa hayaangalii maslahi ya nchi na wananchi wake ndio maana inawawia vigumu kukubali kufanya marekebisho ya msingi ya sheria za nchi kutokana na msingi wa uwepo wa Katiba mpya
Ametolea mfano kupitishwa kwa sheria ya mafao ya wenza wa viongozi kama sehemu ya anasa hizo kwa kuwa sasa mwenza wa Rais mstaafu analazimika kupokea asilimia 60 ya mshahara wa Rais aliyeko madarakani, wakati Rais mstaafu akipokea asilimia 80 ya mshahara huo, hiyo ikienda sambamba na kupatiwa magari yanayobadilishwa kila baada ya muda, walinzi, nyumba na watumishi wengine binafsi.

Post a Comment