Kamati ya Bunge yaridhishwa na mradi wa bilioni nne Misungwi CDTTI

 


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi la ghorofa nne katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Misungwi (Misungwi CDTTI) mkoani Mwanza.

Ni baada ya Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Fatuma Toufiq kafanya ziara ya kukagua mradi huo iliyofanyika Ijumaa Machi 15, 2024.



Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Toufiq amesema utekelezaji wa mradi huo ambao uko hatua ya msingi umefanyika kwa kiwango kinachoendana na thamani ya fedha iliyotumika hadi sasa kiasi cha shilingi Milioni 300.

"Tunaona kazi mnayoifanya ni nzuri, 'value for money' (thamani ya fedha) inaonekana, sisi tukikuta kwenye mradi mambo hayaendi huwa tunabadilika kweli, tukikuta mambo yako vizuri hatuna budi kupongeza" amesema Toufiq akisisita Serikali kutoa fedha kwa wakati ili mradi pia ukamilike kwa wakati.

Naye mjumbe wa Kamati hiyo, Almasi Maige ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Tabora amesema "kwa uzoefu nilionao kwenye mambo ya ujenzi, hapa thamani ya fedha inaonekana, nondo na zenye vyote vimefanyika kwa ubora".

"Msije mkabweteka mkadhani sifa hizi zitaendelea, muendele kusimamia mradi huu hivi hivi hadi utakapokamilika" amesema mjumbe wa Kamati hiyo, Katani Katani ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Tandahimba.


Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Abdulbast Idrisa amesema ujenzi unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 4.27 hadi kukamilika ukijumuisha miundombinu yote ambapo ujenzi ulianza mwezi Juni mwaka huu 2023 ukitarajiwa kukamilika Juni 2025.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Arch. Charles Achuodho amesema chuo kimekuwa kikitoa taaluma mbalimbali ikiwemo uhandisi ujenzi ambayo imeleta tij kwa jamii kutokana na wahitimu wake kushiriki kwenye miradi mbalimbali.

Awali Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis ameipongeza Wizara yake kwa namna inavyoendelea kutenga fedha kwa ajili ya mradi huo wenye uwezo wa kubeba wanafunzi 704 ambapo kwa sasa chuo kina wanafunzi zaidi ya 600 huku mabweni yaliyopo yakiwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 240.

"Nimpongeze Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha nyingi za maendeleo, lakini pia niendelee kumpongeza Mkuu wa Chuo hiki (Misungwi CDTTI) kwa jinsi anavyosimamia vizuri miradi hii" amesema Khamis akiongeza kuwa ujenzi wa mabweni ni muhimu kwani unasaidia kuwalinda wanafunzi na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

No comments