Tufanye haumpendi Paul Makonda, niletee kipenzi chako
KUNA mwandishi mmoja maarufu Tanzania, aliwahi
kusema moja kati ya misemo inayobamba sana nchini hivi sasa, maisha bila
unafiki hajaendi.
Yes, inabidi uwe mnafiki ili maisha, siyo tu
yako mwenyewe, bali hata ya familia yako yaende. Na ajabu sasa, wanafiki katika
nchi hii ndiyo wana maisha mazuri, wanakaa nyumba nzuri, wanaendesha magari
mazuri, wanakula vizuri na wana connection za kufa mtu!
Watanzania wengi wanaishi kisanii licha ya
ukweli kwamba si wengi wenye vipaji hivyo. Nitoe mfano mdogo tu rahisi. Dunia
ina miaka mitatu tu tangu kuondokewa na John Pombe Magufuli. Huyu mwamba
alikuwa mzalendo ambaye mimi binafsi, ukimuondoa Mwalimu Nyerere, nilimkubali
sana.
Akiwa hai, mwenye kiti chake pale Magogoni, kila
mtu aliimba kuhusu utukufu wake, akisifiwa kila kona. Ni katika zama zake,
ndipo tukashuhudia kundi kubwa la wapinzani wake kisiasa, wakiacha kambi zao na
kujiunga naye, wakiunga mkono juhudi zake za kulikwamua taifa. JPM alileta sera
ya Viwanda, akiamini kama nchi ikiwekeza katika sekta hiyo, itajikwamua, siyo
tu kiuchumi, bali hata kuzalisha ajira.
Wateule wake wote wakaimba kuhusu viwanda na
umuhimu wake. Kila mmoja, popote alipokuwa, alisifu na kuchagiza kuwa viwanda
ndiyo njia pekee ya nchi yetu kusonga. Tutasongaje bila umeme wa kutosha? Ndipo
ilipokuja, iwe isiwe, Bwawa la Mwalimu Nyerere lazima lijengwe. Likajengwa!
Agizo likatoka, kila mkoa uwe na viwanda. Kila
Mkuu wa Mkoa ahakikishe, siyo kiwanda, bali viwanda vinajengwa mkoani kwake. Ni
aibu leo kusema, moto ule wa viwanda ulikoishia, ingawa asilimia karibu themanini
ya wateule wake bado wanakula keki ya taifa kwa nyadhifa zilezile alizowapa!
Si kwamba viwanda havipo, vipo lakini ni kama
vile siyo kipaumbele tena. Upepo umebadilika, sasa tupo bize na R4 za mama.
Watu/viongozi wetu hawauishi ukweli wao ndani ya nafsi zao, isipokuwa wanaendeshwa
na upepo, zikija pepo za Kusi, wanaenda nazo, zikianza pepo za Kaskazi,
wanalala nazo mbele!
Kuna mtu anaitwa Paul Makonda, kijana mmoja kada
muaminifu kutoka kule Mwanza. Binafsi nilianza kumfahamu vizuri wakati wa Bunge
la Katiba, miaka ile ya vuguvugu la Katiba mpya ya mzee Joseph Warioba,
lililopata baraka za Rais Jakaya Kikwete.
Katika bunge lile hakuweza kuwa na makeke kwa
sababu alikuwa bado mdogo kiumri na kisiasa, lakini pia asingeweza kufua dafu
kwa hoja mbele ya watu kama akina marehemu Christopher Mtikila.
Lakini alianza kujipambanua yeye binafsi JK
alipompa Ukuu wa wilaya ya Kinondoni. Anajua ni maeneo gani wananchi wanateswa
na kubughudhiwa. Akajitwisha zigo la migogoro ya ardhi. Akafokea utendaji wa
watumishi wa umma, hawa maofisa wa kukaa ofisini kusubiri ripoti!
Na haikua ajabu, JPM alipomkabidhi Mkoa wa Dar
es Salaam. Pamoja na mapungufu anayoweza kuwa nayo kama binadamu, lakini ukweli
usio shaka ni kuwa huyu ni kiongozi mwenye ubunifu, hasa katika kutatua
matatizo ya wananchi. Staili yake ya uongozi, licha ya kuwa haipendwi na
viongozi wenzake, lakini ndiyo hasa Watanzania wanaihitaji.
Pamoja na kukaa kwake nje ya uongozi kwa muda
mrefu, lakini katika kipindi kifupi tu tangu apewe tena kazi, ameendelea kuwa
Makonda yuleyule, mwiba kwa wenzake wanaopenda umangimeza, mwokozi kwa wananchi
waliokata tamaa.
Kama walivyo viongozi wote, Makonda ameishi
uswahilini na anajua maisha yao. Anajua namna wenye fedha (hata zile za wizi)
wanavyotamba. Lakini tofauti na wengine ambao wakipata nafasi hujifanya kusahau
walikotoka, yeye anaendelea kuyaishi yale aliyoishi
Kuna watu (viongozi wenzake na wanufaika wa
mfumo) wanamuona kama mtu anayeongoza bila kufuata taratibu, kwamba hajui
mipaka ya kazi yake, anaingilia kazi za wengine na eti, anapenda sifa. Sijui,
huenda kuna ukweli ndani yake.
Lakini kama kutofuata utaratibu wa utendaji
kazi, kutojua mipaka yake na upendaji wake wa sifa una tija kwa wananchi, kuna
ubaya gani? Hivi kuwa na kiongozi anayefuata taratibu, asiyevuka mipaka yake na
asiyependa sifa, ambaye mwisho wa siku wananchi wanaumia chini yake, ana
umuhimu gani?
Viongozi wanaofuata utaratibu ndiyo wale
wanaowasaidia wenye fedha kuvamia maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa ajili ya
viwanja vya michezo, ujenzi wa shule, zahanati na mambo mengine ya kijamii? Au
ndiyo wale wanaokula na mabepari wanaowanyang’anya viwanja walalahoi?
Kwa sababu unajiuliza, hivi mtu anawezaje kutoka
huko alikotoka na kwenda kuvamia eneo la wazi? Ukimfuata unamkuta ana vibali.
Kavipataje vibali vile kama siyo kwa kusaidiwa na hawa viongozi wanaofuata
taratibu na wasiopenda sifa?
Naomba tuelewane. Siungi mkono aina ya viongozi
wanaofanya kazi kwa kukiuka taratibu zilizowekwa. Katika utawala wa sheria, ni
muhimu sana kuzingatia taratibu kwa sababu hata uhuru tunaoupigania, ni lazima
uwe na mipaka.
Lakini kuna viongozi wanaotumia taratibu hizi
kuumiza wengine. Hawa ndiyo wale ninaowazungumzia. Mtu kadhulumiwa, akienda
polisi, yeye ndiye anaonekana mkosefu, akienda mahakamani anazungushwa na
mwishowe anapokwa haki yake. Sasa akija mtu hapa katikati, akafuatilia na
kugundua ukweli, akivunja taratibu na kutoa haki, kuna ubaya gani?
Unajiuliza, kwa nini watu wanamuona Makonda kama
ndiyo suluhisho badala ya mahakama na vyombo vingine vya utoaji haki? Ni kwa
sababu huko hawapati wanachostahili.
Rais Samia amemsifu Makonda hadharani mara
kadhaa. Hafanyi hivi kwa bahati mbaya. Anaona namna gani wateule wake wengine
wasivyowajibika ipasavyo kiasi kwamba sasa wananchi wanamkimbilia Makonda.
Kitendo cha Rais Samia kuwaambia wakuu wa mikoa
waende wakawajibike kwa wananchi kwa maana wao ndiyo marais wa maeneo yao, ni
dongo kwa wateule wengine wakiwemo makatibu tawala wa mikoa, wilaya,
wakurugenzi wa halmashauri na wateule wengine wote huko, wakiwemo mawaziri.
Hivi kama wote hao watawajibika ipasavyo katika
kuhudumia na kutoa haki, ni nani atakwenda/kumfuata Makonda?
Nchi yetu ina viongozi wabinafsi wanaojijali
wenyewe. Wananchi hawana namna, wanalia lakini machozi yanakwenda na upepo.
Anapojitokeza mtu mmoja akaimba wimbo wao, wanamkumbatia. Unamkumbuka mzee wa
Kiraracha? Kabla yake alikuwepo Edward Sokoine.
Nchi hii inawahitaji watu watatu tu, kwa wakati
mmoja wa aina ya Makonda ili tufike kule tunakotaka, vinginevyo maisha hayako
fair kabisa.

Post a Comment