DKT. BITEKO: RAIS SAMIA AENDELEA KUENZI MAONO YA HAYATI MAGUFULI KWA VITENDO

 


Maono ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya Kitaifa kama Ujenzi wa Bwawa la Nyerere, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Ujenzi wa barabara na madaraja makubwa kama vile Daraja la Kigongo - Busisi yametekelezwa na yanaendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hayo yameelezwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko katika Misa Takatifu ya kumuombea Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Yohana Maria Muzeyi Wilayani Chato Mkoani Geita.

“Niwahakikishie Watanzaniza kuwa miradi yote ambayo Hayati Dkt. Magufuli akiwa Rais wa Nchi yetu, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inaiendeleza yote kwa kasi kubwa ili tumuenzi kwa vitendo”, amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko ameeleza kuwa Watanzania watamkumbuka Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa uwezo wake wa kiuongozi, karama yake ya kutatua changamoto za wananchi pamoja na kuwasikiliza, kuondoa kero mahali penye kero, kuhimiza uwajibikaji Serikalini kwa kuondoa uzembe, ubadhirifu na rushwa.

Misa ya Kumbukizi ya Miaka Mitatu tangu alipofariki Hayati Dkt. John Pombe Magufuli imeongozwa na Makamu Askofu, Padri Ovan Mwenge na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM), ndugu, jamaa na marafiki.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi


No comments