DHAMIRA YA SERIKALI NI KUKUZA UCHUMI WA SEKTA BINAFSI KWA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI: BASHUNGWA
Waziri wa Ujenzi na
Mbunge wa jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa dhamira ya
Serikali ya Awamu ya Sita ni kukuza uchumi wa Sekta binafsi inayochangia
makusanyo ya kodi ambazo zitawezesha ujenzi wa miundombinu ya barabara na
utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo nchini.
Bashungwa amezungumza
hayo Machi 27, 2024 katika kikao kilichowakutanisha wafanyabiashara wa Wilaya
ya Karagwe pamoja na Taasisi za Serikali zinazowahudumia ambapo amesikiliza
kero zao ikiwemo tozo kubwa za kodi, ushuru pamoja na kauli zisizoridhisha
kutoka kwa Maafisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA).
Bashungwa amesisitiza
kuwa ukusanyaji wa mapato unawezesha Serikali kufanikisha malengo yake ya
kuhudumia nchi pamoja na wananchi wake kwa haraka kwa kuwa wajibu wa Serikali
ni kujenga ustawi wa wafanyabiashara na sio kuwadumaza.
“Sijafurahishwa na
madai ya kauli za Maafisa kwa wafanyabiashara ambazo sio sahihi,kwa kuwaaambia wakishindwa kulipa kodi, wafunge baishara, Lengo la Serikali ya Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwawezesha kwa kutoa elimu, kuwashauri na kustawisha
wafanyabiashara” amesisitiza Bashungwa.
Aidha, Bashungwa
ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Kagera kusimamia miongozo
pamoja na kutoa elimu ya Sheria na Kanuni za kodi mara kwa mara kwa
wafanyabiashara pamoja na Maafisa kuwa na kauli nzuri na wezeshi.
Bashungwa amelitaka
Baraza la wafanyabiashara la Wilaya ya Karagwe kutimiza wajibu wao kwa kuitisha
mikutano ya mara kwa mara na wafanyabiashara wote ili kukumbushana masuala tozo
mbalimbali zilizopo na kutatua changamoto zao kwa kuzipatia suluhu ya haraka
kabla mfanyabiashara hajafikia hatua ya kufunga biashara.
Kuhusu utekelezaji wa
miundombinu, Bashungwa amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa barabara
ya Bugene-Benaco (km 128.5) pamoja na kuanza utekelezaji wa barabara ya
Omurushaka - Kyerwa (km 50) na Omugakorongo – Kigarama - Murongo (Km 111) kwa kiwango cha lami.
Naye, Mfanyabiashara
wa Kampuni ya SANOA, Bw. Metisela Philipo ameeleza kuwa kodi na faini
wanazotozwa zimekuwa kubwa na haziendani na biashara wanazozifanya hivyo
kupelekea baadhi ya wafanyabiashara kufunga biashara zao.
Kwa upande wake, Kaimu
Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Bw. Omary Kigoda amesema kuwa suala la lugha
mbaya kwa walipa kodi sio msimamo wa Taasisi hivyo TRA itaendelea kuwachukulia
hatua baadhi ya watumishi ambao wanaenda kinyume na maadili ya utumishi.
Mwenyekiti wa Chama
cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Karagwe, Paschal Rwamugata amesema kuwa moja ya
majukumu ya Chama ni kusikiliza kero za wananchi na kuitaka Serikali kutatua
kero hizo kama ambavyo imekuwa ikifanya.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi

Post a Comment