BASHUNGWA AWAPA SIKU 4 TANROADS KUKAGUA BARABARA NA MADARAJA YOTE NCHINI
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa siku nne kwa Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) nchi nzima kufanya tathmini na ukaguzi wa madaraja, makalvati na barabara kuu zote ambazo zimekuwa zikifanyiwa matengenezo ya mara kwa mara na kuwasilisha taarifa hizo kwa wakuu wa Mikoa ili ziweze kuchukuliwa hatua ya haraka.
Agizo hilo amelitoa
mkoani Lindi Machi 5, 2024 kutokana na taarifa ya Mamlaka ya hali ya hewa
kuhusu maoteo ya mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali na
kuathiri miundombinu ya barabara, madaraja na makalvati kwa baadhi ya maeneo.
“Nielekeze hadi kufika Machi 9 Mwaka huu kila Meneja wa Mkoa wa TANROADS na timu yake wakabidhi taarifa ya hali ya barabara na maeneo ya hatari yanayoweza kujitokeza katika madaraja na makalvati ili Serikali iweze kuchukua hatua za haraka”, amesisitiza Bashungwa.
Kwa upande wake Mkuu wa
Mkoa wa Lindi, Zainab Telack ameomba fedha za dharura za matengenezo ya
barabara kufika kwa haraka ili ziweze kunusuru barabara zilizoathiriwa na mvua
na zile zilizofunga hasa kwa wananchi wa Wilaya ya Liwale ambao wamekuwa
kisiwani hawawezi kutoka wala kuingia.

Post a Comment