WAZIRI MKUU AAGIZA KIGOGO SERENGETI AKAMATWE
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, ACP Salum Morcase kumkamata Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Bw. Saad Mutunzi Ishabailu kwa kosa la kuhamisha sh. 213,748,085 kwa awamu nne kwa njia ya uhamisho wa ndani kwa kushirikiana na watumishi wa OR TAMISEMI na kuzitumia kwa matumizi yao binafsi.
“Mkamate huyo bwana sasa hivi aende polisi akafunguliwe mashtaka, huyu ni wa kupeleka mahakamani moja kwa moja. DPP aelezwe afungue jalada la mashtaka. Wale wenzake tumewapeleka mahakamani tayari sababu tulibaini walihusika na wizi kama huu kwenye Manispaa ya Kigoma mwaka jana.”
Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumanne, Februari 27, 2024) wakati akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwenye kikao kilichofanyika katika kwenye Halmashauri hiyo, mkoani Mara.
Waziri Mkuu amefikia hatua hiyo baada ya kuwaeleza watumishi na madiwani mbinu wanazotumia watumishi wachache wa baadhi ya Halmashauri ambao walikuwa wanashirikiana na watumishi watatu wa kitengo cha Treasury Single Account (TSA) kuiba fedha za umma.
Akitolea mfano juu ya mbinu zinazotumika na wachache hao, Waziri Mkuu aliwaeleza watumishi wa Halmashauri hiyo pamoja na Madiwani kwamba Juni 10, 2023 walitumia mwanya wa kuombea kibali fedha za bakaa kwa barua iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Chatta Luleka, kwenda Hazina.
“Ilipofika Juni 30, walikuwa wamemaliza kutumia fedha hizo na ikabakia sh.milioni 9 lakini kwa kuwa walishaandika barua ya kuomba kibali, bado fedha hizo zilihamishwa na kuingizwa kwenye akaunti ya Halmashauri tarehe 19 Juni 2023 na aliyejua alikuwa Bw. Ishabailu peke yake. Hakutoa tarifa kwa Mkurugenzi, Mwenyekiti wala wakuu wa idara.”
“Nilituma timu yangu hapa ije kufanya uchunguzi, ikawahoji baadhi ya watumishi akiwemo Ofisa Mipango wa Halmashauri, Bw. Wilfred Mwita ambaye alisema hajui uwepo wa hizo fedha wala hawakuwa na mpango wala bajeti inayohitaji hizo fedha. Mkurugenzi wa sasa, Bw. Furaha alipoulizwa naye alisema hajui uwepo wa hizo fedha, kwani alianza kazi Agosti, mwaka jana.

Post a Comment