Serikali kuwalipa wanaopisha ujenzi wa barabara
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imesema ulipaji wa fidia kwa wananchi ambao mali zao zinaathiriwa na miradi ya Ujenzi wa barabara hufanyika kwa Mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya Bungeni jijini Dodoma leo Februari 13,2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu, aliyeuliza Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya malipo ya fidia kwenye Miradi ya Barabara za TANROADS zinazopita kwenye makazi ya watu Kibamba.
Eng. Kasekenya amefafanua kuwa wananchi wote ambao mali zao ziko nje ya eneo la hifadhi ya barabara wanalipwa fidia na wale ambao mali zao zimo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara hawastahili kulipwa fidia.
Amesisitiza suala hilo ni kwa wananchi wote nchi nzima ikiwemo wananchi wa Jimbo la Kibamba.
Aidha Eng. Kasekenya ameeleza kuwa Barabara ya Kibamba Shule - Mpiji Magohe imeanza kujengwa kwa awamu na itakuwa barabara ya mzuguko wa Nje (Outer Ring Road) ya mkoa wa Dar es Salaam.

Post a Comment