Mwijaku awaacha watu midomo wazi ombi lake kwa Madame President

 

Chawa anayejipatia wafuasi wengi mitandaoni kwa tabia zake zisizo za kawaida, ambaye pia ni muajiriwa wa kampuni kubwa ya habari ya Clouds Media, Mwijaku, mwishoni mwa wiki iliyopita aliwaacha watu midomo wazi, baada ya kutoa ombi lisilotarajiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kupitia akaunti yake kwenye mtandao wa Twitter, ambao siku hizi unafahamika kama X, mtangazaji huyo aliandika kuwa endapo atatangulia kufa kabla ya Madame President, basi anamuomba kiongozi huyo wa kitaifa ahudhurie mazishi yake.

Bila kutoa sababu za ombi hilo, Mwijaku aliiomba familia yake kuzingatia wosia huo, huku akimsisitiza Rais Samia kuzingatia ombi lake.

Kufuatia andiko hilo, mamia ya watu walitoa maoni yao, wengi wakionyesha kushangazwa kwao na jambo hilo, wakidai limevuka mipaka kwani kwa umri wake, ni wazi jambo hilo ni uchuro.

Aidha, wengine pia walisema ombi hilo limezidi kiwango cha uchawa, kwani huenda alikosa jambo la kusema kiasi cha kujikuta ametoa ombi hilo tata. Mwijaku amejizolea umaarufu mkubwa baada ya kujiingiza kwenye uchawa, tabia mpya ambayo inapendwa na watu wengi, hasa vijana ambao maisha yao yanategemea kusifia wengine!

No comments