DRC yaiomba jamii ya kimataifa kutumia vikwazo kuweka shinikizo kwa Rwanda ili iache 'kuunga mkono M23'
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaiomba Jumuiya ya kimataifa kuiwekea Rwanda vikwazo vikali, ikiituhumu kuwasaidia waasi wa M23 inayopigana nao mashariki mwa nchi hiyo, ili usalama uweze kurejea katika eneo hilo.
Rwanda inakanusha kuwasaidia M23, na inashutumu DR Congo kufanya kazi na kundi la waasi wa Rwanda wanaoendesha harakati zao mashariki mwa nchi hiyo (FDLR), ambalo inasema ni kinyume na serikali ya Rwanda. DR Congo pia inakanusha madai hayo.
Katika mahojiano ya Kiingereza na BBC Newsday , msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Patrick Muyaya alisema kuwa kamwe hatajadiliana na kundi la M23, ingawa limesema liko tayari kushiriki katika mazungumzo ya amani.
Muyaya alisema: "Tunachoomba jumuiya ya kimataifa ni rahisi. Ni kwamba wanaweza kutumia vikwazo kuweka shinikizo kwa Rwanda kuacha kile inachofanya mashariki mwa DRC."
Muyaya pia amesema kuwa ziara mbili za Goma ndani ya wiki moja za Waziri wa Ulinzi Jean-Pierre Bemba, zilikuwa sehemu ya mpango kwamba "tunafanya kila linalowezekana" kuhakikisha usalama wa watu wa Goma na Sake.
Katika kipindi cha wiki za hivi karibuni, mapigano makali kati ya M23 na jeshi la Congo (FARDC) na washirika wao kama vile jeshi la SADC, yamejikita katika viunga vya mji wa Sake, ambao uko umbali wa kilomita 25 kaskazini magharibi mwa Goma.

Post a Comment