DMDP II KUJENGA BARABARA, MASOKO NA STENDI DAR ES SALAAM
OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) awamu ya pili utajenga barabara za lami katika Mkoa wa Dar es salaam kilomita 250, kuanzisha mfumo wa udhibiti wa taka ngumu, masoko 18 pamoja na vituo vya mabasi tisa.
Mhe.Mchengerwa ameyasema hayo leo Februari 20, 2024 jijini Dar es salaam kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa fedha za mradi huo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia ambapo waliotia saini ni Waziri wa Fedha na Mpango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete.
Akizungumza baada ya kusainiwa mikataba hiyo, Waziri Mchengerwa amesema Jiji hilo limekuwa na changamoto ya miundombinu, ikiwamo ya barabara, ambapo awamu ya kwanza ya DMDP iliboresha jumla ya kilometa 207 katika Halmashauri tatu zilizokuwa chini ya mradi na imeleta mabadiliko makubwa.

Post a Comment