BASHUNGWA ATAKA MUAROBAINI WA BARABARA KUHARIBIKA KABLA YA MUDA
Waziri wa Ujenzi,
Innocent Bashungwa amewaagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kutafuta
ufumbuzi kuhusu suala la kuharibika kwa barabara kabla ya muda uliopangwa ili
kuokoa fedha za Serikali zitakazotumika kurekebisha miundombinu hiyo.
Agizo hilo amelitoa
jijini Dodoma Februari 14, 2024 katika kikao cha 19 cha Baraza la Wafanyakazi
wa TANROADS na kuwasisitiza kusimamia miradi kwa weledi na uzalendo ili
kusaidia miradi kukamilika kwa viwango na kwa wakati.
“Suala la kuharibika
kwa barabara kabla ya wakati ‘pre-mature
failure’ ni tatizo, hakikisheni mnapambana nalo, chukueni hatua za kisheria
kwa Mkandarasi atakayetekeleza mradi chini ya kiwango”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameagiza TANROADS kutumia kikamilifu mtambo wa Ukaguzi wa Barabara (Road Scanner) wakati wa kufanya ukaguzi wa miradi ya barabara na madaraja na hata kutumia vifaa vingine
vitakavyoweza
kuwasaidia kubaini ubora wa mradi mapema kabla ya kukabidhiwa.
Ameielekeza TANROADS
kuimarisha na kukijengea uwezo Kitengo chake cha Usimamizi wa miradi (TECU), ili
kusimamia miradi kwa weledi na ufanisi.
Kadhalika, Bashungwa
ameitaka TANROADS kusimamia sheria ya uzito wa magari barabarani na kutoa faini
au adhabu nyingine kwa yeyote atakayekiuka sheria hiyo kwa mujibu wa sheria pamoja
na kuwaelekeza Maafisa wanaofanya kazi kwenye mizani kutii na kufuata sheria
kama inavyoelekeza ili kuzilinda barabara nchini.
“Hakuna kiongozi wala
mtumishi ambaye yupo juu ya sheria, hata mimi siwezi kumsaidia yeyote
anayekiuka sheria hii, atakayekiuka achukuliwe hatua na sio kunipigia simu”,
amesema Bashungwa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta, amemhakikishia
Waziri Bashungwa kutekeleza maagizo aliyowapa na kuendelea kufanya kazi kwa ari
na bidi katika utendaji wao wa kila siku ili kuleta tija kwa Wakala huo.
Naye, Mweyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na
kazi nyingine (TAMICO), Eng.
Nchama Wambura, amesema wataendelea kushrikiana na kufanya kazi kwa bidii ili
kuleta mabadiliko chanya na maendeleo kwa utekelezaji sahihi na ubora kwa
miradi wanayoendelea kutekeleza nchini.
Mkutano wa 19 wa Baraza la wafanyakazi la TANROADS, umefanyika Dodoma
kwa Siku 2 na kushirikisha zaidi ya wajumbe 100 kutoka Mikoa yote nchini.
Imetolewa na Kitengo cha Mwasiliano Serikalini, Wizara
ya Ujenzi.

Post a Comment