Baba Levo mbona kama sijamuelewa kuhusu milioni kumi?

 


Nimemsikia Msanii, Mtangazaji na Chawa, Baba Levo akiongea kuhusu namna alivyokorofishana na kupigwa na msanii mwenzake, Harmonize. Kwamba walikuwa Casino moja kubwa Bongo, KondeBoy akiwa kama ameburudika flan hivi.

Anasema wakiwa hapo, tajiri mmoja mcheza kamari, alipata fedha za kutosha. Baada ya kupata, akamfuata Baba Levo na kumpatia shilingi milioni kumi. Akamwambia mbili achukue yeye, halafu zinazobaki awagawie wenzake, ambao miongoni mwao alikuwepo Harmonize, Rayvany na madairekta kadhaa.

Lakini ghafla akajitokeza Harmonize, akampora shilingi milioni tano na akasema yeye anachukua hizo zote, na kwamba wenzake wagawane hiyo milioni tano iliyosalia. Kwamba kukatokea mtafaruku uliosababisha kijana toka Mtwara amkwide mwenzale wa Kigoma hadi kumsababishia maumivu.

Sikusikiliza hadi mwisho ilikuwaje, lakini kufikia hapo ni dhahiri kulikuwa na tafrani baina yao, jambo ambalo linanipa maswali lukuki.

Kwanza, najiuliza, simulizi hii ni ya kweli au kama kawaida, Baba levo anatafuta tension mitandaoni? Maana kwa namna alivyojipambanua, msanii huyo ni mzuri zaidi kwa vichekesho kuliko kazi yake ya sanaa tuliyomfahamia awali.

Na inapokuwa ni kweli, je, Harmonize, kwa namna tunavyojua kupitia simulizi zake mitandaoni, ni mtu wa kugombea milioni tano? Kwamba yeye Baba Levo, ambaye siku chache nyuma aliwahi kujinadi kuwa yeye ni msanii namba tatu tajiri Tanzania, anaweza kupewa ‘chips’ za milioni kumi agawane na wana Casino?

Yaani Rayvany, ambaye tunaambiwa aliilipa Wasafi kiasi cha shilingi bilioni moja na ushee ili ajiondoe, leo hii anakuwepo katika kundi la watu wanaosubiri mgao wa milioni kumi kutoka kwa tajiri aliyeshinda kamari Casino?

Nashawishika kuamini maneno ya Ney wa Mitego aliyezungumza hivi majuzi kuwa mashabiki wasiyachukulie siriaz maisha ya wasanii mitandaoni, kwamba wengi wanaishi kwa kuigiza, siyo maisha yao halisi.

Yaani msanii tajiri namba tatu Tanzania, yupo Casino anageuka chawa wa wacheza kamari? Harmonize, ambaye amekaririwa mara nyingi akijinadi kuwanunulia magari wasichana anaotoka nao, leo anavizia na kupora chips Casino?

Kama maisha ya wasanii wetu ndiyo haya, basi tuendelee tu kumuombea Diamond Platinum aendelee kuwaonyesha wenzake njia, maana hata kama na yeye anaigiza, angalau tunaona anachokifanya kwenye uwekezaji.

Tukio hili, kama Baba Levo anadhani amemuaibisha Harmonize, anajidanganya kwa sababu ukweli ni kwamba limeidhalilisha sanaa yote ya Bongo Fleva, maana Harmonize na Rayvany ndiyo nembo ya muziki huo sasa hivi. Kama hao wanaweza kuwemo katika orodha ya wanaosubiri mgao wa milioni kumi, vipi kuhusu LavaLava, Mboso, Ibrah na D Voice? 

No comments