Alex Msama mwekezaji mzawa aliyegoma kutoweka licha ya mawimbi mazito baharini

 

                                                        


NI ukweli usiopingika kwamba miaka angalau kumi iliyopita, kulikuwa na changamoto nyingi sana miongoni mwa wafanyabiashara, wazawa na wageni kote Tanzania. Watu walishuhudia biashara nyingi zikifungwa, hususan viwanda, mahoteli, miradi ya kilimo huku wafanyabiashara wamiliki, wengi wakianguka kiuchumi.

Ni kipindi ambacho pia kilishuhudia wafanyabiashara matajiri wa michongo, yaani wale ambao walifanya vitu nje ya pazia, kwa maigizo, wakipotea kwenye ramani hasa baada ya mikakati mipya ya udaiji kodi, kufuata taratibu za kibiashara na udhibiti mkubwa wa fedha za serikali, uliofanywa na uongozi wa awamu ya tano ya nchi, chini ya Rais John Pombe Magufuli.

Alex Msama Mwita, mmoja wa wawekezaji wazawa ambaye ameibuka akitokea chini kabisa na kuwa miongoni mwa watu wachache waliotengeneza ajira kwa watanzania wenzao, licha ya kukumbwa na tufani hiyo ya mtikisiko mkubwa wa kiuchumi, lakini ameendelea kubakia huku nchi ikishuhudia mamilionea wengi wakitoweka.

Akiwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Dira Media Group, moja kati ya vyombo vya habari maarufu nchini Tanzania, vikimiliki Radio, Magazeti na Televisheni, Msama alitoa ajira nyingi kwa vijana katika eneo hilo, wakiwemo waandishi, watu wa matangazo na idara zingine nyingi. Lakini pia, Alex, kada kindakindaki wa Chama Cha Mapinduzi, ndiye muasisi wa Tamasha maarufu zaidi la dini nchini Tanzxania, Tamasha la Pasaka.

Tamasha hilo kabla ya mwaka 2016, lilikuwa likifanyika kila mwaka, likiwakusanya pamoja wasanii wengi wa nyimbo za Injili nchi nzima katika jukwaa moja, ambalo pia lilikuwa likifanyika katika mikoa kadhaa, kitendo ambacho kiliwapa nafasi waimbaji hao kuonyesha uwezo wao, lakini pia kupata fursa ya kujiingizia maokoto.

Kwa muda mrefu, majukwaa ya muziki Tanzania yalitawaliwa na muziki wa Bongo Fleva, Muziki wa Dansi na Taarafu, huku muziki wa Injili ukiwa umesahauliwa kabisa. Katika ubunifu wa aina yake, muasisi huyo aliwakusanya waimbaji hao, kuanzia chipukizi hadi nyota kabisa na kuwapa nafasi ya kuweza kushindana na waimbaji wengine nyota kutoka kote Afrika Mashariki.

Shughuli hiyo ya kila mwaka nayo ilikuwa ikizalisha ajira nyingi kwa vijana na watu wazima kupitia ujenzi wa majukwaa, usafiri, vyakula na vinywaji katika viwanja vote vilivyotumika kwa ajili ya shughuli hizo. Ni tamasha ambalo liliweza kuwaleta watu maarufu Afrika kama kundi la Kwetu Pazuri toka Rwanda, waimbaji Solomon Mukubwa wa DRC na wengineo kadhaa.


                                   
Alex Msama akiwa na mwanasiasa maarufu nchini Kenya, Raila Odinga

Msama ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Msama Auction Mart na Msama Music Center, baada ya kimya cha muda mrefu wa kutofanyika kwa tamasha hilo la Pasaka, amesema shoo hiyo itafanyika mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

"Litakuwa ni tamasha la kufungua awamu mpya baada ya kusimama kwa muda mrefu. Nina uhakika zile shangwe ambazo watu wa Mungu walikuwa wakizipata, zitawarudia tena kwani hadi hivi sasa, tayari wasanii wa Injili kutoka mataifa nane wamethibitisha kushiriki.

"Kwa kiwango kikubwa maandalizi muhimu yamekamilika na nina uhakika mashabiki wa Dar es Salaam watapata kile walichokikosa kwa muda mrefu. Uzuri wa Tamasha la mwaka huu, lina kauli mbiu ya Kumshukuru Mungu kwa kuiletea nchi Rais mama yetu, Samia Suluhu Hassan," anasema Msama wakati akizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni.



No comments