Mbunge Kigwangalah adai kufuatiliwa
Siku chache baada ya kudai kuwepo kwa kigogo ndani ya Serikali ya Tanzania kununua jumba lenye thamani ya shilingi bilioni 25 huko Dubai na mwingine kununua nyumba huko Masaki yenye thamani ya dola milioni sita, Mbunge wa Nzega vijijini, Hamis Kigwangalah, amedai anafuatiliwa.
Katika akaunti yake ya X, zamani Twitter, Kigwangala ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Afya na Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema ameshtushwa na suala hilo kwa vile hana uadui na mtu, na hakumtaja mtu.
"Kujaribu kuninyamazisha haitosaidia kitu maana kama unahisi mimi najua kitu, ambacho sijakisema, jua na wengine wanajua!"
"Kama umeficha vizuri, hakuna litakalokupata, maana TAKUKURU ama sekretariet ya maadili watataka ushahidi usio na shaka kabla ya kukupeleka kortini. Na siku zote ushahidi hautopatikana, na hivyo kama Jamhuri hatutokupata! Kama wewe ni kiongozi, jiulize tu ukishaiba mali nyingi sana ya umma unasikia raha gani? Utapeleka wapi? Utatumia zote hizo? Utazikwa nazo?
"Halafu jiulize, mwenye kosa ni anayetoboa mtumbwi ama anayepiga yowe na kumsonteshea mtoboaji ili wasafiri wote tushtuke? Tumdhibiti?
"Kushtuka shtuka namna hii inaonesha watu wanajishuku. Kunifuatilia na kutafuta kunitisha tisha mtanifanya nichambue hadharani taarifa za CAG, za TAKUKURU na michango ya wabunge bungeni nk. Humo kuna viashiria vingi sana vya rushwa na ubadhirifu, je kama Taifa mifumo yetu ya uwajibikaji imefanya kazi ipasavyo?
"Nilipozungumza juu ya uwepo wa haja ya kuimarisha mifumo ya uwajibikaji na usimamizi wa mali ya umma, sikuwa na nia ya kumtaja mtu yeyote. Nilipenda kutoa maoni yangu tu juu ya haja ya kuimarisha mifumo/taasisi za uwajibikaji kama Taifa; aidha mifumo/taasisi za kifedha, na mifumo/taasisi za kisiasa. Kama hujaitazama ile interview, nenda kaitazame."

Post a Comment