Mo Dewji awashukuru waliomuombea alipotekwa miaka mitano iliyopita
Kupitia mtandao wa X ambao zamani ulifahamika kama Twitter, mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Singida alisema atawashukuru milele wale wote waliomuombea.
Mtiririko wa matukio kutekwa Mo
OKTOBA 11
Mfanyabiashara maarufu nchini, ambaye pia ni mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji (Mo Dewji) alitekwa na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha za moto, saa 11 alfajiri wakati akiingia kufanya mazoezi katika gym ya Colosseum, Oysterbay jijini Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Kinondoni, Jumanne Muliro, athibitisha tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema Polisi Dar inafuatilia madai ya kutekwa kwa mfanyabiashara huyo maarufu nchini.
Dereva wa Uber aliyekuwa amefika hotelini hapo kumchukua mteja wake alinukuliwa akisema kwamba aliona watu wanne wakishuka kwenye gari dogo, wakiwa wamejifunika usoni, wakapiga risasi moja juu na kumchukua Mohammed Dewji.
Baada ya muda, Mambosasa alisema kwamba waliomteka Mo ni Wazungu wawili na msako mkubwa unafanywa kwa raia wa kigeni wote waliopo nchini kutokana na tukio hilo. Mchana; Mambosasa alibainisha kuwa watu watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano kuhusu kutekwa kwa Mo Dewji.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paulo Makonda alitoa onyo kali kwa yeyote atakayeibuka na kuanza kusambaza taarifa za uongo kuhusiana na tukio hili au kuligeuza na kulifanya mtaji wa kisiasa.
OKTOBA 12
Msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara, alikamatwa na kuzuiliwa kwa mahojiano kuhusiana na sakata la kutekwa kwa mfadhili wa timu hiyo, Dewji.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Mambosasa alisema Manara anashikiliwa kutokana na kusambaza taarifa za tukio hilo la kutekwa kwa Mo kwenye mitandao kwa madai ya kutumwa na familia, bila kutumwa na familia hiyo.
“Hajatumwa na familia hivyo tunamshikilia,” alisema Mambosasa.
Watu 12 wanashikiliwa na jeshi hilo kutokana na tukio hilo huku uchunguzi ukiendelea.
OKTOBA 13
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alizungumza na vyombo vya habari nchini na kubainisha kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kumtafuta mfanyabiashara huyo pamoja na watu wengine wanaodaiwa kupotea.
Alibainisha kuwa tayari watu 20 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano kuhusiana na sakata hilo ili kuweza kuwabaini wahusika. Pia alieleza kuwa amewaagiza polisi kutowashikilia zaidi ya saa 24 wale watakaobainika kutokuwa na mahusiano na tukio hilo.
OKTOBA 14
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Injinia Hamad Masauni, alisema serikali inatarajia kufunga kamera maalumu za CCTV katika miji mikubwa na baadhi ya mikoa nchini ili kukabiliana na uhalifu.
Masauni alipoulizwa uwezekano wa kuomba msaada nje ya nchi ili kufanikisha kukamata wahalifu alikataa na kusema wachunguzi wa ndani ya nchi wanatosha.
OKTOBA 15
Familia ya Mohamed Dewji ilitangaza donge nono la Sh bilioni moja kwa mtu yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa mtoto wao huku wakiahidi kumlinda mtoa taarifa.
Familia ilitangaza namba za simu zitakazotumika kukusanya taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa Mo.
Akisoma taarifa iliyotolewa na familia, Azim Dewji, ambaye alijitambulisha kama msemaji wa familia akiwa ameongozana na baba mzazi wa Mo, Gulam Hussein Dewji, alisema familia inasikitishwa na tukio la utekwaji wa kijana wao na kwamba yeyote atakayetoa taarifa za upatikanaji wa kijana huyo familia itampatia kiasi hicho cha fedha.
OKTOBA 16
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa watu 19 kati ya 26 waliokuwa wanashikiliwa na polisi wakihusishwa na utekaji wa Mo Dewji wameachiwa kwa dhamana akiwemo Haji Manara.
OKTOBA 19
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwa kutumia kamera za CCTV wamebaini gari lililotumika kumteka Mo Dewji.
Alisema gari hilo aina ya Toyota Surf liliingia nchini Tanzania kutoka nchi jirani ambayo hakuitaja jina Septemba Mosi, 2018, likiendeshwa na Obasanjo Zacharius Junior.
Namba za usajili wa gari hilo ni AGX 404 MC, ni gari ambalo polisi wanaamini lilitumika kumteka Mo Dewji katika Hoteli ya Colosseum Alhamisi, Oktoba 11.
Sirro amesema kwa kutumia CCTV wamebaini kwamba gari hilo aina ya Surf baada ya kutoka Hoteli ya Colosseum, lilipita barabara za Haile Sellasie, Ali Hassan Mwinyi, Maandazi, Mwai Kibaki na kisha likapotelea kwenye eneo la Mlalakuwa karibu na mzunguko wa Kawe.
“Bado watu wetu wanafuatilia kuona kama walielekea maeneo ya Silver Sands au Kawe. Hapo ndipo tunaamini gari hilo lilipotelea, tunakwenda jumba kwa jumba kutafuta,” alisema Kamanda Sirro.
Katika hatua nyingine, Kamanda Sirro amebainisha kuwa kati ya watu wanane ambao wanaendelea kuwashikilia wakati wakichunguza tukio hilo, ni kapteni wa boti. Lakini hakusema ni wa boti gani, na inayofanya safari zake maeneo gani, japo awali polisi walisema wameimarisha ulinzi wa mpaka katika Bahari ya Hindi kuzuia Mo kutoroshwa nchini.
Mpaka sasa bado hazijajulikana sababu za Mo kutekwa na nani hasa ambao wamemteka. Awali ilidaiwa kuwa Mo ametekwa na Wazungu wawili jambo ambalo IGP Sirro alikataa kukubali ama kukanusha akisema hilo ni suala la kiupelelezi zaidi.
Sirro alisema bado hawajui alipo Mo, lakini walibaini kuwa waliomteka walikuwa na bastola ambazo ni za kufyatua risasi za ukubwa wa 9mm.
OKTOBA 20
Katika ujumbe ulioandikwa kwenye ukurasa wa twitter wa Kampuni ya Mohamed Enterprise Tanzania Limited (MeTL), ulisema: “Namshukuru Mwenyezi Mungu nimerudi salama nyumbani. Nawashukuru Watanzania wenzangu na watu wote kote duniani kwa dua na sala zao. Nashukuru mamlaka zote, namshukuru Rais Magufuli, likiwemo Jeshi la Polisi, zilizofanya kazi ya kuhakikisha narudi salama.”
Ujumbe huo uliandikwa saa 09:15 alfajiri baada ya Mo Dewji kupatikana.
Alfajiri hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba:
“Mohammed Dewji amerudi salama. Nimezungumza naye kwa simu dakika 20 zilizopita. Sauti yake inaonyesha yu mzima bukheri wa afya. Shukrani kwa wote kwa dua na sala. Naenda nyumbani kwake kumuona muda huu.”
Aliandika ujumbe mwingine uliosema:
“Nimemuona na kuongea kwa kirefu na Mohammed Dewji. Ni mzima wa afya isipokuwa ana alama za kufungwa kamba mikononi na miguuni. Mnamo saa nane usiku, watekaji waliamua kumtupa kwenye maeneo ya viwanja vya Gymkana. Naamini Polisi watatoa taarifa za ziada kuhusu kilichojiri.”
Kamanda Mambosasa aliyefika nyumbani kwa Dewji kuthibitisha kurejea kwake nyumbani, alisema watu waliomteka Mo Dewji walikuwa na lafudhi ya mojawapo ya lugha za mataifa ya Afrika Kusini, kwamba hatua hiyo imethibitisha wazi hakutekwa na Watanzania.
“Nataka kuuthibitishia umma wa Tanzania kwamba nimefika nyumbani kwa kina Mo Dewji, nimeongea naye niko na kikosi cha makachero hapa na ndugu yetu ni mzima kama IGP alivyozungumza na umma kwamba Jeshi la Polisi litaendelea na uchunguzi ili kuhakikisha kwamba tunampata mhusika akiwa mzima,” anasema Mambosasa.
Wakati huohuo, gari ambalo linaaminika kutumika katika kumteka Mo, limepatikana kando ya viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam ambapo bilionea huyo aliachwa.
Hata hivyo, zamu hii lilionekana likiwa na namba za usajili wa Tanzania T 314 AXX.
Hakuna mtu aliyekamatwa, na bado haijulikani watu waliomtelekeza Mo eneo hilo walitumia usafiri gani kuondoka katika eneo la tukio. Sambamba na hilo, hakuna majibizano ya risasi baina ya watekaji na Polisi, lakini watekaji hao wametelekeza gari likiwa na silaha ya kivita aina ya AK47 na bastola tatu.
IGP Sirro amewaambia waandishi wa habari kuwa waliomteka Mo Dewji walifanya hivyo kwa lengo la kujipatia pesa.
Sirro amesema bilionea Mo aliwapa namba ya simu ya baba yake mzazi mzee Gulam ili waongee naye juu ya hilo, lakini hawakupiga simu wakihofia kunaswa na polisi.
“Mohammed Dewji amesema watekaji hao walikuwa na wasiwasi sana, walimwambia wanataka pesa, alipowauliza shilingi ngapi hawakusema. Aliwapa namba ya simu ili waongee na baba yake, lakini waliogopa kwa sababu wanafahamu ulinzi wetu ni imara na tungewakamata,” alisema IGP Sirro.
Amesema kuwa watu waliokuwa wakimshikilia Mo walikuwa watatu, wawili walikuwa wakiongea Kiingereza na mmoja akiongea Kiswahili kidogo.
Polisi nchini Tanzania wamesema watafanya kila wawezalo kuwatia nguvuni watu waliomteka na kumshikilia bilionea Mohammed Dewji, Mo, kwa siku tisa.
IGP Sirro aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuachiwa kwa Mo ni mwanzo wa kuwanasa wahalifu hao na kuwapata wakiwa wazima au wamekufa.
“Mbio ukizianza sharti uzimalize. Huu ni mwanzo tu. Hao wahalifu wanaotaka kuchafua jina la nchi yetu lazima tuwatie nguvuni,” amesema Sirro.
Amesema upelelezi umeimarishwa kwa kushirikiana na mtandao wa Polisi wa Kimataifa (Interpol).
“Nataka niwaambie wahalifu yawezekana wananisikiliza hivi sasa kuwa popote watakapokwenda tutawanasa. Wakienda Afrika Kusini tunao, Kenya tunao, Uganda tunao hata Msumbiji, popote pale tutawakamata, maana tayari tuna ushirikiano na wenzetu,” amesema Sirro.

Post a Comment