Mbunge Kalist apokea mitambo ya kuchimba visima virefu Mwenyekiti CCM akishuhudia
16 Desemba, 2024.
Mkuu wa Wilaya Lushoto Mhe. Kalist Lazaro ameongoza zoezi la Kupokea Mtambo wa Kuchimba Visima Virefu vya Maji unaokwenda kupunguza changamoto za maji katika maeneo zaidi ya 14 ya Kata mbalimbali Wilayani Lushoto.
Zoezi hilo limeshuhudiwa na M/Kiti CCM Wilaya ya Lushoto Ally Kassim Daffa aliyemshukuru M/Kiti CCM Taifa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ununuzi wa mitambo hii ya Kuchimba Visima. M/Kiti Daffa ameendelea kuishukuru Wizara ya Maji kupitia Naibu Waziri wa Maji Mhe. Marry Prisca Mahundi aliyekuwa ziarani Lushoto Januari 06 hadi 10, 2024 ambapo miongoni mwa maelekezo ya Naibu Waziri ilikuwa ni kuletewa Mtambo kuanza Kuchimba Visima Wilayani hapa.
M/kiti amewataka Viongozi, wanasiasa na wananchi kuwaacha wataalamu wa RUWASA wafanye kazi yao ya Kitaalamu bila kuingiliwa.
Nae DC Kalist Lazaro ameungana na M/Kiti CCM Wilaya kuwaonya wanasiasa kutoingilia zoezi hilo kwa kusema...
_"Kazi ya kuchimba visima ni kazi ya kitaalamu. Sitegemei kiongozi wa kisiasa au wa aina yoyote kuja kuelekeza RUWASA mahali pakuchimba kisima. Sitaki kusikia watu wanavutana"._
Aidha, DC Kalist Lazaro amesema kakuwa visima vitavuta maji kwa kutumia nishati ya umeme, miradi itakapokamilika wananchi watalazimika kufuata utaratibu wa uchangiaji gharama za uendeshaji ili kulipia umeme na mahitaji mengine kama watakavyoelekezwa kwa mujibu wa sheria.
Wakati huo huo, Meneja RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga aliyeonyesha utayari mkubwa kupambana na shida za maji ameainisha maeneo yatakayoanza kuchimbwa visima 14 kwamba ni pamoja na:-
Magamba Coast, Dochi, Kwemakame, Mziragembei, Mshangai, Mategho, Kwekanga Sokoni, Makole, Ungo, Lwandai Mlola, Kweulasi, Sunga, Mbaru na Gare.
DC Kalist amewataka RUWASA kuzingatia maelekezo ya Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ya hivi karibuni kutaka mitambo itumike kuchimba visima vitakavyodumu kwa miaka mingi bila kuharibika kwani lengo la Dkt. Samia ni kutatua changamoto na si kuhadaa wananchi.

Post a Comment