Arnold Schwarzenegger akamatwa kutokana na kodi ya saa ya kifahari
Arnold Schwarzenegger alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Ujerumani kwa madai ya kushindwa kutangaza saa ya kifahari aliyokuwa akipanga kuipiga mnada kwa ajili ya kutoa misaada.
Muigizaji huyo wa Hollywood alizuiliwa kwa saa tatu katika uwanja wa ndege wa Munich siku ya Jumatano.
Uchunguzi wa madai ya kukwepa kulipa kodi ulianzaiswa baada ya kubainika kwamba saa hiyo ilinuiwa kuuzwa ndani ya Umoja wa Ulaya (EU).
Kulingana na sheria za Umoja wa Ulaya, mtu yeyote anayefika na "pesa au vitu fulani vya thamani" zaidi ya €10,000 (£8,580) lazima atangaze.
Hata hivyo, chanzo kiliiambia CBS News, mshirika wa BBC wa Marekani, kwamba Schwarzenegger hakuulizwa kujaza fomu ya kutangaza alichobeba.
Muigizaji, mwanasiasa na mwanaharakati huyo wa mabadiliko ya hali ya hewa hatimaye aliweza kulipa kodi, lakini tu baada ya kukabiliana na matatizo kadhaa.
Baada ya mashine ya kadi kutofanya kazi, iligundulika kuwa benki ya karibu ilikuwa imefungwa na ukomo wa kutoa ATM ulikuwa chini sana, ikimaanisha kuwa mzee huyo wa miaka 76 alilazimika kusubiri mashine mpya ya kadi kuletwa na maafisa wa forodha, chanzo kilisema.
Msemaji wa muigizaji huyo aliliambia gazeti la udaku la Ujerumani Bild kwamba tukio hilo la uwanja wa ndege lilikuwa "mzaa uliojaa makosa, lakini ungweza kutengeneza filamu ya kuchekesha ya polisi ".
Bild ilisema "alichukua tukio hilo kwa utulivu" na picha iliyochapisha ilionyesha Schwarzenegger akitabasamu akipiga picha na kushikilia kisanduku cha saa na barua inayosema " ni ya Austria".
Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, saa hiyo ilitengenezwa maalum kwa ajili ya nyota ya Terminator na mtengenezaji wa saa wa kifahari Audemars Piguet, ambaye hutengeneza saa ambazo zinaweza kuuzwa kwa mamia ya maelfu ya dola.
Saa hiyo ilisemekana kupigwa mnada katika chakula cha jioni cha kuchangisha fedha kwa ajili ya The Schwarzenegger Climate Initiative huko Kitzbuhel, Austria, takriban kilomita 89 (maili 55) kutoka Munich, baadaye siku ya Alhamisi.
Taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu hafla hiyo, inayotarajiwa kufanyika katika hoteli ya nyota tano ya Stanglwirt, ilisema "kazi za sanaa, maonyesho yaliyotiwa saini, na uzoefu kutoka kwa ulimwengu wa michezo na filamu" zitauzwa.
Orodha ya mnada wa saa hiyo, iliyopatikana na Bild, ilisema ni moja kati ya 20 zilizopo, na itajumuisha "picha ya Arnold katika pozi lake la kitambo lenye maneno 'Arnold Classic'". Bei ya kuanzia ya mnada ilikuwa €50,000.

Post a Comment