Vita vya Ukraine: Wimbi la mashambulizi ya anga ya Urusi yaripotiwa kote Ukraine
Urusi imeanzisha wimbi la mashambulizi katika miji kadhaa kote Ukraine katika mashambulizi ya usiku kucha.
Tahadhari ya anga ya nchi nzima iliwekwa wakati ndege zisizo na rubani na makombora zilipiga Kyiv, Odesa, Dnipropetrovsk, Kharkiv na Lviv mapema Ijumaa.
Nchini kote, watu kadhaa walijeruhiwa na mtu mmoja aliuawa, ripoti zinasema.
Mashambulizi hayo ya usiku wa kuamkia leo yamekuja siku chache baada ya Ukraine kuipiga meli ya kivita ya Urusi katika bandari ya Feodosia ya Crimea.
Mashambulizi hayo yanaonekana kuwa makubwa na yameenea katika miji mingi nchini kote. Kharkiv iko chini ya kilomita 40 (maili 25) kutoka mpaka wa mashariki wa nchi hiyo na Urusi, wakati Lviv iko katika magharibi ya mbali ya Ukraine, kilomita 70 tu kutoka mpaka wa Poland.
Meya wa Kyiv Vitali Klitschko alisema kwenye Telegram kwamba ulinzi wa anga katika mji mkuu ulikuwa ukifanya kazi kuzima shambulizi hilo, na kuwataka raia kukaa katika makazi yao.
Meya wa Kharkiv Igor Terekhov alisema mtu mmoja aliuawa na watu kadhaa kujeruhiwa katika mfululizo wa mashambulizi katika mji huo.
Huko Odesa kusini, meya wa jiji hilo aliripoti kuwa jengo limeshika moto baada ya kushambuliwa na ndege isiyo na rubani.
Meya wa mji wa magharibi wa Lviv Andriy Sadovyi alisema kumekuwa na takribani mashambulio miwili katika jiji hilo.
Shambulio hilo la Urusi linakuja siku moja baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kuishukuru Marekani kwa msaada wake wa mwisho wa kijeshi wa $250m (£195.7m) ulioidhinishwa, ambao ulijumuisha silaha za ulinzi wa anga.

Post a Comment