Mtaka awataka viongozi Makambako kutosumbua wananchi
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amewataka viongozi wa serikali wilaya ya Makambako kuacha usumbufu kwa wananchi wanaojitafutia kipato na badala yake wawe na mipango thabiti ya kusimamia maendeleo ya mji huo.
Mtaka amesema hayo wakati akisikiliza na kutatua kero za wananchi kwenye mkutano wa hadhara aliouandaa katika uwanja wa Stendi ya Zamani, Makambako.
Katika mkutano huo, amesisitiza weledi kwa watumishi wa umma wanaowahudumia wananchi badala ya kuwa na urasimu na vitendo vya rushwa katika maeneo yao ya kazi.
Aidha, ameagiza kufanyika uchunguzi wa tuhuma dhidi ya watumishi wa kituo cha afya Makambako ambapo wamelalamikiwa na wananchi kutoa huduma mbaya pamoja na vitendo vya rushwa.
Mtaka ameuandaa mkutano huo wa kusikiliza kero za wananchi akiwakusanya wataalamu wa idara mbalimbali za wilaya hiyo ili kutafuta ufumbuzi kwa changamoto zinazowakabili wananchi.

Post a Comment