Mkurugenzi wa Uchimbaji Visima aondolewa kwa kutofika Hanang baada ya Mafuriko
Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemuondoa kwenye nafasi yake Mkurugenzi wa
Sehemu ya Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa, Mhandisi Mashaka
Sitta baada ya Mhandisi Sitta kutotimiza vema majukumu yake katika eneo
hili muhimu la uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa na usimamizi wa
mitambo na zaidi kutofika Wilayani Hanang Mkoa wa Manyara baada ya
kutokea changamoto ya mafuriko yaliyosababisha vifo 80, majeruhi na
uharibifu wa miundombinu ikiwemo ya maji licha ya Maboss zake akiwemo
Waziri Aweso kufika Hanang.
Kufuatia mabadiliko haya Aweso amemteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi
wa RUWASA Mhandisi Ndele Mengo kuchukua nafasi hiyo ya Sitta na
amemuelekeza Mhandisi Ndele kufika mara moja Wilayani Hanang na kuanza
kazi ya usimamizi wa uchimbaji wa visima kwa maeneo ambayo miundombinu
ya maji imeathiriwa na mafuriko.
Aweso amesema mabadiliko haya yamelenga kuimarisha sehemu ya uchimbaji
wa visima na ujenzi wa mabwawa na kusisitiza kuwa mchakato wa uundwaji
wa Wakala kamili wa DDCA unaendelea na utakamilika kwa wakati.
Katika hatua nyingine Waziri Aweso amemteua Mhandisi Mariam Majala kuwa
Mkurugenzi Msaidizi wa Ufundi, RUWASA, kabla ya uteuzi huo Majala
alikuwa Meneja wa RUWASA mkoa wa Simiyu na amemteua pia Mhandisi Abbas
Pyarali kuwa Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Usanifu na Usimamizi wa
Miradi ya Maji Wizara ya Maji, awali alikuwa Mhandisi Mkuu katika Idara
ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Wizara ya Maji.
Waziri Aweso amefanya uteuzi huu kwa mamlaka aliyonayo kupitia Sheria
Namba 5 ya Mwaka 2019 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira.
Jamii Forum

Post a Comment