Marekani yaishutumu Iran kwa kuhusika na mashambulizi ya Houthi katika Bahari Nyekundu
Marekani imeishutumu Iran kwa kuhusika na mashambulizi ya waasi wa Houthi kutoka Yemen dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari Nyekundu, ikisema Tehran inawaunga mkono kwa kutoa ndege zisizo na rubani, makombora na taarifa za kijasusi.
Madai hayo ambayo yanatokana na taarifa za kijasusi za Marekani, yanaendeleza kauli nzito za Marekani kuhusiana na uwezekano wa jukumu la Iran katika mashambulizi hayo kufikia sasa.
Msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa Adrienne Watson alisema katika taarifa yake siku ya Ijumaa, "Tunafahamu kwamba Iran inashiriki kwa kina katika kupanga operesheni dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari Nyekundu."
Amesisitiza kuwa "uungaji mkono wa Iran kwa Wahouthi ni mkubwa na unajumuisha utoaji wa zana za hali ya juu za kijeshi, usaidizi wa kijasusi, misaada ya kifedha na mafunzo," na kwamba Tehran "imekabidhi maamuzi ya kiutendaji kwa Houthis."

Post a Comment