Bongo Fleva inasogea, fedha zinazidi kumiminika

 



Muziki wa kizazi kipya hakika umepiga hatua kubwa, kwani tofauti na hapo mwanzo, sasa majina ya wasanii wetu yanatajika sehemu kubwa ya bara la Afrika na pengine sehemu zingine za dunia.


Bado hatujawa na msanii wa ngazi ya kidunia, lakini angalau tunao wasanii  wanaoweza kupigiana simu na wasanii hao wa kidunia na wakaongea mambo yao.


Ni kama tunavyokua taratibu katika soka. Leo, pale Taifa Stars, kocha akiamua anaweza kupanga kikosi kizima kutokana na wachezaji wanaocheza nje ya Tanzania, kitu ambacho miaka michache nyuma kisingeweza kutokea.


Wakati ule, mwanzoni kabisa mwa miaka ile ya tisini, tulianza kutengeneza wasanii ambao walifahamika kiwilaya, kimikoa na kikanda, tatizo kubwa likiwa ni teknolojia ya mawasiliano.


Ni kipindi ambacho tulikuwa na redio moja tu, RTD, ambayo nayo kutokana na wingi wa majukumu, ulinzi wa utamaduni na maadili, haukuupa uzito muziki huu, kwa ile dhana ya muda mrefu huko nyuma, kwamba ni uhuni.


Ikumbukwe, vijana wengi walianza kufanya muziki huu kwa kuiga nyimbo za Marekani, wakigeuza mashairi kutoka Kiingereza kuleta Kiswahili na wengine kwa kuingiza mashairi yao kufuatisha midundo ya nyimbo za kizungu.


Kuanzishwa kwa kituo cha redio cha Redio One, miaka ile ya tisini, ni moja ya kichocheo kikubwa cha kuanza kupata umaarufu kwa muziki huu na ndipo wakati ambao wasanii wa ngazi ya kitaifa walianza kupatikana.


Na pale mwanzo, wasanii wengi walijiunga kimakundi na ndiyo maana kulikuwa na makundi mengi, tofauti na sasa ambapo wengi wanapenda kuimba solo.  Si rahisi kuwataja wote, lakini angalau tukaanza kuwasikia Kwanza Unit, Hard Blasters Crew, Gangstar With Matatizo, Hot Pot Family, TMK Wanaume Family, B Love M, East Coast Team, Mabaga Fresh, Daz Nundaz, Ngoni Tribe, Watu Pori na Gangwe Mob.


Pia kulikuwa na wale wana wa Uswahilini Matola, East Zoo, Solid Ground Family, Wateule, Unique Sisters, Xplastaz, Tip Top Connection, Dar Skendo Halla, Mandojo na Domokaya, Wagosi wa Kaya na mengineyo mengi.


Pamoja na uwingi wa wasanii wa makundi, pia kulikuwa na wasanii kadhaa solo, ambao nao walianza kupata umaarufu mkubwa ambao kwa uchache wao ni pamoja na Too Proud (Sugu), Dola Soul, Mike T, Mac D, Afande Sele, Profesa Jay, Lady Jay Dee, Stara Thomas, Zay B, Rah P.


Taratibu, muziki huu ukaanza mwendo na kwa kasi ya ajabu, makundi yakaanza kufifia, watu wakajitoa na kufanya kivyao vyao.

Huu ndiyo msimu ambao tulipata wasanii wengi maarufu, kila mmoja akingÕara kwa wakati wake kabla ya kumpisha mwenzake.


Zilikuwepo zama za Juma Nature, zilikuwepo enzi za Mr Nice, zikaja nyakati za Ray C, akasumbua sana Ferooz, MB Dogg, Joslin, Dudubaya, TID, Mr Ebbo, Chid Benz, Bushoke, Ngwair, kwa kuwataja wachache.


Lakini kwa nyakati zote hizo, wapo wasanii ambao walidumu kwa umaarufu, wakitoa kazi baada ya kazi na hivyo kufanya uwepo wao kutokuwa wa msimu. Na hawa ndiyo wasanii tunaoweza kuwaweka daraja lao, la hadhi ya juu kama Greatest Of All Time.


Hapa utamkuta Sugu, Profesa Jay, Lady Jay Dee, Juma Nature, Mwana FA, AY, Inspekta Haroun, King Crazy GK, Fid Q, Joh Makini, Mr Blue, Dully Sykes, Ngwair na wenzao wachache wa kariba yao.


Ni kipindi ambacho wasanii wengi waliuchukulia muziki kama sifa, wachache wakaufanya kuwa maisha, na baadhi yao wakaamua kuachana nao ili washughulike na mambo mengine. Na ni nyakati hizi, wasanii wachache mno walifikiria kuhusu kufanya wimbo na msanii wa nje, ukimuondoa Sugu na AY ambao walifanya uthubutu huo.


Uanzishwaji wa vituo vingi zaidi vya redio binafsi vilichangia sana kukua na kusambaa kwa muziki huu, hongera nyingi sana kwa Clouds FM, ambao waliamua, kwa makusudi kabisa, kuubeba na kuufanya kuwa kitambulisho chao. 


Kadiri njia za mawasiliano zilivyokuwa zikiongezeka, ndivyo na wasanii wetu nao walivyokuwa wakizidi kujazana na kuufanya muziki huu kukua na kuanza kubadili maisha yao.

Kwamba muziki ni maisha na ajira kubwa pia, ni kauli ya siku nyingi kutoka kwa waasisi wa Bongo Fleva, lakini kuigeuza kauli hii katika uhalisia wake ilichukua miaka mingi hadi kuja kutimia. Namna msanii wa muziki wa kizazi kipya anavyotazamwa leo ni tofauti kabisa na miaka kumi iliyopita. 

Muimba muziki wa sasa anachukuliwa kama tajiri. Asante kwa teknolojia kusogea karibu zaidi. Tofauti na zamani ambako ili msanii asikike na apate hela ni lazima apeleke kazi yake redioni na apande kwenye majukwaa, leo hii, anaweza kupandisha kazi yake kwenye platforms za muziki na akajipatia fedha za kutosha.

Hata hivyo, ni kukosa heshima kutomtaja Diamond Platnumz katika hili. Huyu ndiye msanii aliyetafsiri kwa vitendo kuhusu utajiri ulioko kwenye muziki, akaliona soko la nje na fursa zake na akatumia kipato chake siyo tu kuwainua wasanii wengine, bali kufanya uwekezaji ambao leo unamtofautisha pakubwa na wasanii wengine.

Unapomsikia msanii ambaye hana ukubwa wa Diamond kwa mfano, akisema milioni hamsini ni hela ndogo, unataraji kwamba ana kiasi cha fedha za kutosha. Wasanii wawili waliotoka katika lebo ya Diamond ya WCB, Harmonize na Rayvanny, wanathibitisha fedha zilizoko katika muziki.

Harmonize aliilipa lebo hiyo shilingi milioni 600 na Rayvanny akafanya malipo mara mbili ya hapo ili awe mbali nao. Kama hao vijana ambao Diamond aliwakuta hawana hata senti tano waliweza kulipa mamilioni hayo ya shilingi, unawaza nini kuhusu Ali Kiba, Lady Jay Dee, Profesa Jay, Banana Zoro, Mwana FA, AY, Madee, Joh Makini, Dully Sykes, Jay Melody, Mr Blue, Jux, Marioo, Mbosso, Nandy, Billnas, Mimi Mars, Maua Sama na wengine wanaotamba sasa?








No comments