Raia wa Canada achagua kubaki Gaza ili kurekodi matukio ya vita




  1. Baba mmoja Mpalestina mwenye uraia wa Canada ameamua kusalia Gaza, licha ya kwamba hatimaye aliruhusiwa kuondoka katika eneo lenye vita.

    Mansour Shouman aliambia BBC kwamba anahisi kuwajibika kubaki na kuandika matukio yanayomzunguka.

    Alisema watoto wake watano na mkewe ni miongoni mwa raia wa Canada wa kwanza ambao walifanikiwa kuvuka salama hadi Misri siku ya Jumanne.

    Kati ya Wakanada 80 walioidhinishwa kuondoka Gaza hadi sasa, 59 wametoka salama.

    Global Affairs Canada imesema kuwa wanafahamu zaidi ya raia 400 wa Canada, wakaazi wa kudumu na wanafamilia wao wanaotaka kuondoka kupitia kivuko cha Rafah kuelekea Misri.

    Bw Shouman, mshauri wa usimamizi, alisema kuwa kwake kubaki nyuma ni wajibu.

    "Mradi watu milioni 2.3 wanateseka, ninaamini kuwa ni wajibu wangu wa kidini, wajibu wangu wa kibinadamu kukaa na kusimulia hadithi kuhusu kile kinachotokea," alisema.

    "Naweza kuzungumza Kiingereza, nimeishi Magharibi," alisema Bw Shouman, ambaye tayari amezungumza na vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na BBC.

    Bw Shouman ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Malkia huko Kingston, Ontario na Chuo Kikuu cha Calgary huko Alberta, na amefanya kazi kwa miaka kadhaa katika sekta ya mafuta na gesi ya Alberta.

    Mwenye asili ya Jerusalem, Bw Shouman alisema kuwa yeye na familia yake walichagua kuhamia maeneo ya Palestina yaliyokaliwa kwa mabavu miaka miwili iliyopita ili watoto wake waishi katika nchi ya mababu zao.

    Walichagua kuishi Gaza, alisema, kwa kuwa ni mji alikozaliwa mke wake.

    "Tumekuwa tukiishi maisha mazuri sana hapa," Bw Shouman alisema, licha ya machafuko ya muda mrefu katika ukanda wa Gaza.

    "Watoto wetu walikuwa wakienda shule za kimataifa," alisema. "Mimi na mke wangu tulikuwa tukifanya kazi. Tulikuwa na marafiki wengi. Msikiti wa eneo hilo ulikuwa mzuri."

    Lakini aliongeza yeye na familia yake hawakutarajia kamwe kuwa katikati ya vita vya sasa.

    Sasa, Bw Shouman amefanya hospitali katika Khan Younis kuwa nyumba yake, ambapo analala katika chumba kidogo karibu na wadi ya uzazi.

    "Kila mtoto mchanga anapozaliwa, mimi husikia habari njema," alisema.

    Kivuko cha mpaka cha Rafah kati ya Gaza na Misri kilifunguliwa Jumatano ili kuruhusu idadi ya raia kuondoka. Mamia ya wamiliki wa pasipoti za kigeni, wakiwemo zaidi ya Wamarekani 400, wamevuka mpaka kufikia sasa. Ilikuwa ni fursa yao ya kwanza kufanya hivyo tangu vita kuanza tarehe 7 Oktoba.

    Orodha ya wanaoruhusiwa kuvuka imekubaliwa na Misri na Israeli. Kisha, nchi husika zinaarifiwa ili kuhakikisha ziko tayari kupokea raia wao.


z

No comments