Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya
Uchukuzi imetumia zaidi ya shilingi bilioni mbili kununulia mtambo
maalum wa kidigitali wa kunyakulia mizigo (Crane Simulator) ili
kurahisisha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosoma kozi za
uendeshaji mitambo katika wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI).
Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Mkuu wa
Chuo cha DMI Dkt. Tumaini Gurumo amesema elimu ya uendeshaji wa
mitambo unahitaji wahitimu kufanya mazoezi ya nadharia na vitendo ili
kuwezesha kuwa mahiri katika utendaji.
“Kozi za uendeshaji wa mitambo hususani kwenye mitambo ya
kunyakua vitu vizito zinahitaji uzoefu kwenye nadharia na vitendo hivyo
kupitia mtambo huu wanafunzi watatakiwa kufuzu kwenye maeneo yote
ili kuwezesha kufanya kazi kwa weledi, tunaishukuru sana Serikali ya
awamu ya Sita kwa kuwezesha jambo hili” alisema Dkt. Tumaini.
Dkt. Tumaini amesema Serikali imeendelea kutoa fedha kwa chuo cha
DMI lengo likiwa kuhakikisha chuo hicho kinazalisha wataalam
watakaoweza kushindana sokoni lakini pia kuweza kuendesha miradi
mikubwa inayotekelezwa nchini hasa miradi ya ujenzi wa meli katika
maziwa Nchini.
Kwa upande wake Mkufunzi wa DMI, Elinathan Blasius amesema
mtambo huo wa kisasa unaotumia teknolojia ya kompyuta
utawawezesha wahitimu kwenda na wakati hasa kwenye upakiaji na
upakuaji wa mizigo katika bandari, Viwandani na kwenye migodi.
Kwa upande wake Mwalimu Leonard Mwesiga ametoa rai kwa
wanafunzi wanaopenda kujiunga na kozi hiyo kutuma maombi ili
kuongeza wataalam kwenye eneo la uendeshaji mitambo.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Uchukuzi)
Post a Comment