BASHUNGWA AAGIZA WAHANDISI KUJENGEWA UWEZO
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameiagiza Bodi ya Usajili wa
Wahandisi (ERB) kuiwezesha na kuiendeleza taaluma ya kihandisi ili kuongeza
ushindani katika Soko la ndani na nje ya nchi.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo jijini Dodoma mara baada ya kuzindua jengo jipya la Bodi hiyo “Mhandisi Annex” ambalo limejengwa na wahandisi wazawa.
Bashungwa amesema kuwa Serikali bado ina uhitaji mkubwa wa wahandisi
kwani Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anahakikisha anaifungua nchi kutokana
na uwekezaji mbalimbali anaofanya kupitia miradi mbalimbali, kwa namna moja ama
nyingine wahandisi wanahitajika kwa wingi ili kutekeleza miradi hiyo.
“ERB muendelee kusimamia taaluma hii, Watanzania tunaitegemea katika
kuendeleza nchi yetu, tuijenge nchi yetu katika namna ambayo mchango wa
Mhandisi utaonekana katika kuifanya Tanzania ipendeze na kuwa sehemu ya
kuigwa”, amesema Bashungwa.
Bashungwa ameiagiza Bodi hiyo kuhakikisha inaandaa mpango mkakati wa kuwajengea uwezo wataalamu wake ili waweze kutekeleza miradi hiyo na kuweza kuleta tija kwao na Taifa kwa ujumla.
Aidha, ameiagiza Bodi hiyo kuendelea kuiheshimu na kuitendea haki
taaluma hiyo kwa kuhakikisha miradi wanayoitekeleza inakuwa bora na yenye
viwango.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Eng. Menye Manga, ameahidi
kuyafanyia kazi maelekezo ya Waziri huyo ambapo amesema kuwa watahakikisha
wanafuata, sheria, kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu yao.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini, Wizara ya Ujenzi.

Post a Comment