SERIKALI INAFANYA MABORESHO MAKUBWA KATIKA KILIMO-MAJALIWA
WEPO wa chakula cha kutosha ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa lolote kwa kuwa bila ya kuwa na uhakika wa chakula hata usalama wa nchi nao huyumba, hivyo ni vyema kujiwekea mikakati ya kuzalisha chakula cha kutosha/
Katika kudhihirisha umuhimu wa usalama wa chakula nchini, hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani lililofanyika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) kuanzia Oktoba 16, 2023 hadi Oktoba 20, 2023.
Mkutano huo wa wakuu wa nchi na Serikali ulimbatana na maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani pamoja na maadhimisho ya miaka 78 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO)
Jukwaa hilo ambalo liliwakutanisha wadau wa kilimo wakiwemo vijana, wakulima, wazalishaji wadogo, watunga sera, wawekezaji katika kilimo na wanasayansi duniani, wote wakiwa na lengo la kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa chakula ili kufikia mustakabali bora wa chakula kwa wote.
Akizungumza katika jukwaa hilo Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeweka mipango inayolenga kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi na ziada kuuza nje ifikapo 2030.
Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kuhakikisha mipango hiyo inafanikiwa, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara na nishati vijijini ili kurahisisha shughuli za kilimo. “Maboresho mengine ni ujenzi wa viwanda vya kuzalisha pembejeo za kilimo na kuhamasisha wakulima kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji.”
Waziri Mkuu alisema licha ya jitihada za kuboresha sekta ya kilimo ambazo zimewekwa ndani za kushirikisha vijana na wanawake kuhakikisha kwamba wanaongeza teknolojia, kutumia mbolea kwenye kilimo, pamoja na ushirikishaji wa sekta binafsi, pia Serikali ameamua kuungana na FAO kupitia Mkurugenzi Mkuu na ameahidi kuiunga mkono mipango hiyo.
Mheshimiwa Majaliwa alisema katika kuhakikisha Taifa linafanikiwa kwenye utekelezaji wa mpango wake wa kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula, Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeanza kupanua wigo wa kilimo kutoka cha kutegemea mvua na kujikita zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji, ambapo imetenga shilingi bilioni 900.
Waziri Mkuu alisema kuwa mbali na maboresho hayo yaliyofanyika katika sekta ya kilimo, pia Serikali inawasimia wakulima kuanzia hatua za awali za maandalizi ya mashamba, upandaji wa mazao, uvunaji na uhifadhi wa mazao hayo hadi kwenye utafutaji wa masoko kupitia maafisa ugani ambao wapo hadi vijijini.
Alisema Serikali imeanza kusajili wakulima katika mfumo wa kidigitali lengo likiwa ni kujua idadi ya wakulima, ukubwa wa mashamba na aina ya mazao wanayolima ili kurahisisha ufikishwaji wa huduma za ugani. “Kilimo ndio maisha, kilimo ndio chakula, tunataka kujikita zaidi katika kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia mabwawa yetu. Tunataka tujiridhishe kuwa hakuna Mtanzania atayekufa kwa kukosa chakula.”
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), Dkt. Qu Dongyu alisema Tanzania ina fursa kubwa ya kuendeleza sekta ya kilimo na uchumi wa buluu, hivyo Shirika lao liko tayari kushirikiana na Tanzania katika kutoa msaada wa kitaalam pamoja na kukuza mifumo ya uzalishaji wa chakula.
Aidha, Dkt. Qu Dongyu alisema kuwa Shirika hilo limevutiwa na mradi wa kuwawezesha vijana unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania wa Jenga Kesho Iliyobora “Building Better Tomorrow” (BBT). “FAO tutaunga mkono mradi huu ili Serikali ya Tanzania iweze kutimiza malengo ya kuwainua vijana na wanawake kwenye sekta ya kilimo kama ilivyo moja ya agenda kwenye mkutano wa FAO wa mwaka 2023”.
Mkurugenzi huyo wa FAO amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sekta ya kilimo pamoja na kuboresha mahusiano na mashirika ya kimataifa, ambapo ameahidi kutembelea Tanzania mwaka 2024 kwa ajili ya kujionea maendeleo katika sekta ya kilimo pamoja na kupanua wigo wa majadiliano kati ya Tanzania na Shirika hilo ili kuendelea kuwezesha zaidi sekta ya kilimo na uchumi wa Buluu.
Naye, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamata Shaame Hamisi alisema kwa sasa Serikali inafanya maboresho makubwa katika sekta ya kilimo na miongoni mwa maboresho hayo ni utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji ambayo inalenga kuimarisha upatikanaji wa chakula.
Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema Serikali imeendelea kuwashawishi vijana kushiriki katika shughuli za kilimo kwani mbali na kuongeza uzalishaji wa chakula, pia kilimo ni miongoni mwa sekta zinazotoa ajira nyingi, hivyo watakuwa wamejihakikishia ajira.
Licha ya kuhudhiria alimuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani na maadhimisho ya miaka 78 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), pia Waziri Mkuu alifungua katika Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia lililofanyika Palazzo Regione Lombardia, Milan nchini Italia pamoja na kutembelea shamba la kisasa la ufugaji wa ng’ombe.

Post a Comment