FAMIILIA YA MTANZANIA ALIYETEKWA INA MATUMAINI JAPO HOFU PIA WANAYO

 

Familia ya mmoja wa watanzania wawili wanaoshikiliwa mateka na kundi la Hamas huko Gaza, Clemence Felix Mtenga imesema wana matumaini juu ya ndugu yao kurejea salama japo pia bado kuna wasiwasi na mashaka juu ya mustakabali wake

Mtanzania mwingine anayeshikiliwa mateka ni Joshua Loitu Mollel. Wawili hao ni wanafunzi wa mafunzo ya kilimo kwa vitendo. Walitekwa Oktoba 7 wakati wa mashambulio ya Hamas kwa Israel kisha Israel kuanzisha mashambulizi ya kulipa kisasi.

Dada wa Clemence, Neema Christina Mtenga, ameiambia BBC taarifa mpya za kutajwa kwa majina ya waliotekwa akiwemo ndugu yao zimewapata matumaini mapya kuliko awali lakini hiyo haimaanishi wasiwasi umeondoka kabisa.

“Kiukweli kwa sasa siwezi kusema kwamba tuna ahueni sana lakini kidogo baada ya kuzungumza na ubalozi kuna taarifa tulipewa ambazo zilitutia matumaini kulinganishana hapo awali. Balozi wa Tanzania aliyepo Israel aliwasiliana na baba na alichotuambia ni kwamba Clemence ni mmoja wa watu ambao hawaonekani na kuna namna ambavyo anafanya ili kumpata”

Neema, ameongeza kuwa: “Kwa kweli, kila mtu ana mashaka, ana huzuni, ukizingatia kuwa ni mdogo wetu na ni juzi tu amekwenda na hali ukiangalia katika vyombo vya habari inatia mashaka, hakuna mtu ambaye anaweza kulala vizuri. Kwa kweli sijui nielezeje lakini ni hivyo”.

Hata hivyo, amesema “Tunaamini kwamba kwa uwezo wa Mungu watarejea kulingana na taarifa tunazopata kuopitia machapisho mbalimbali kw ani miongoni mwa waliotekwa na Hamas, kwa hiyo tunaamini kwamba kwa huruma ya Mungu ndugu yetu atarejea salama”.

Akimzungumzia Clemence kitabia na mwennedo amesema ni mtu mtulivu, anayefanya mamabo yake kwa umakini pia mtaratibu na kwa sababu ya utulivu huo ndiyo maana wanapata mashaka juu ya hali yake huko aliko kwa sasa na kwamba wangependa apate ujumbe kuwa wanampenda na wanamuombea usiku na mchana.

No comments