Absa Bank Tanzania Kuwekeza Zaidi Katika Huduma Zake Za Kidigitali
Benki ya Absa Tanzania imesema itaendelea kufanya uwekezaji
mkubwa zaidi kupitia huduma zake za kibenki kwa njia za kidigitali ili kufanya
huduma za kibenki nchini kupatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu na hivyo
kuwafikia watu wengi zaidi.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam leo na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo
Bwana Obedi Laiser wakati akizundua wiki ya huduma kwa wateja akisema kuwa
wamejipanga katika kuhakikisha wateja wao wanapata huduma zenye viwango vya
kimataifa wawapo katika matawi yao nchini kote ama wawapo nje ya matawi kwa
kutumia huduma za kidigitali.
“Tunajivunia wateja wetu, ninyi ndio msingi na sababu ya sisi kuwepo, tumewaita
ili tukae pamoja na kuwasikiliza ni namna gani mngependa tuwahudumie, lakini
lililo kubwa zaidi ni kutumia muda huu kuwashukuru kwa msaada na ushirikiano
wenu wa kibiashara.
“Kwa niaba yangu na timu nzima ya benki yetu tunaahidi kuendelea kuwahudumia
vizuri kwa huduma bora na za kiubunifu zinazokidhi mahitaji yenu ya kibenki,”
Bwana Laiser akawaambia baadhi ya wateja waliohudhuria hafla hiyo.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa benki hiyo, Bi. Ndabu Lilian Swere
alisema Absa imekuwa ikitoa huduma zake kwa kiwango cha juu sawasawa na maoni
ya wateja kama ambavyo wamefanya katika mwaka huu kwa kuingiza bidhaa na huduma
mbalimbali tofauti sokoni.
Akitaja baadhi ya huduma, Bi Ndabu alitaja huduma za mikopo hususani mikopo ya
nyumba iliyoboresha ambapo sasa mteja anaweza kujenga ama kununua nyumba kutoka
taasisi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya nyumba walizoingia nazo
makubaliano. “Kingine kilicho kizuri baada ya kusikia maombi ya wateja wetu
tumeweza kurekebisha mikopo yetu isiyo na dhamana ambapo wateja wetu wanaweza
kukopa hadi sh milioni 150 kwa masharti nafuu kabisa bila kusahau huduma yetu
ya Absa Wakala tuliyoizindua hivi karibuni ambayo wateja wetu wanaendelea
kufurahia ofa ya miezi miwili ya kufanya miamala kwa mawakala wetu bila ada,”
alisema Bi. Ndabu.

Post a Comment