TASAC NA ZMA ZAPEWA HEKO
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bi. Salama Mbarouk amelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Nchini (TASAC) na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) kwa kuendelea kutoa elimu ya fursa zilizopo kwenye sekta ya bahari ili kuhakikisha zinatumika kwa kuzingatia usalama.
Akizungumza wakati akifungua warsha maalum ya wadau wa bahari ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Bahari Duniani yanayofanyika Kitaifa Mkoa wa Kusini Pemba, Mkuu wa Mkoa huyo Bi. Salama amesema pamoja na fursa hizo kuna faida za kiuchumi zinazoweza kupatikana endapo wananchi hao watatumia vyema fursa ya uwepo wao katika visiwa vya Pemba.
"Nawapongeza sana TASAC na ZMA kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kutoa elimu wananchi hawa sababu wanaweza kuwa wanaishi katika kisiwa hiki wasizione fursa zilizopo kwenye bahari lakini pia wasijue matumizi sahihi ya fursa hizo, hivyo nina Imani elimu mtakayowapa wataitumia ipasavyo kwenye fursa mtazowaeleza’ amesema Mkuu wa Mkoa Bi. Salama Mbarouk.
Mkuu wa Mkoa Bi. Salama amesema ili kuhakikisha usalama na mazingira ya bahari vinazingatiwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mapinduzi Zanzibar zimeendelea kuchukua hatua stahiki kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara kupitia Taasisi zake za udhibiti ili kuhakikisha sheria zinazoongoza usafiri na matumizi ya bahari zinazingatiwa kwa mustakabali wa vizazi vya sasa na badae.
Aidha, Mkuu wa Mkoa Bi. Salama ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanakuwa mabalozi kwa kuwaelimisha wengine elimu watakayoipata mara baada ya warsha hii kukamilika.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Uchukuzi, Bi. Stella Katondo amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Bi. Salama Mbarouk kuwa Serikali zote mbili zitaendelea kushirikiana kwenye maeneo yote ili kuhakikisha watumiaji wa bahari wanazingatia sheria za kimataifa zinazosimamia usafiri majini na bahari kwa ujumla.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Nahodha Ernest Bupandwa ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wanafunzi wa kike wanaosoma masomo ya sayansi kujiunga na chuo hicho ili kuongeza idadi ya wataalaam katika sekta ya bahari nchini.
Madhimisho ya Wiki ya bahari duniani kitaifa yanayofanyika Mkoa wa Kusini Pemba yanatawajiwa kuhitimishwa 28 Septemba 2023 ambapo kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu ya ‘Miaka 50 ya MARKPOL Uwajibikaji Wetu Unaendelea’.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Post a Comment