CHAUREMBO PALASA: WATU WASIOJUA NGUMI WANADIDIMIZA NDONDI NCHINI
Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBRC) Chaurembo Palasa amesema licha ya mchezo wa ngumi kupendwa na watu wengi, lakini hauwezi kuendelea kwa vile watu wenye nafasi ya kuweza kuusogeza mbele hawaujui.
Palasa ambaye pia ni bondia mkali wa zama zake, aliiambia Ojuku Blog kuwa watu wenye mamlaka serikalini, ambao ndiyo wenye dhamana ya kuupambania mchezo huo, hawasikilizi maoni ya watu wanaoujua mchezo huo, isipokuwa wanawajali wanaopiga majungu kwa faida yao binafsi.
Palasa (kushoto) akiwa na Promota Hamis Haruna.
"Nimeshajaribu sana kuongea na watu hawa, walio katika Baraza la Michezo au hata serikalini, hawaelewi. Ukiwaambia wanakuona hujui kitu, lakini majungu yasiyo na faida kwa ngumi wanasikiliza sana. Kama serikali ingetia nia ya dhati katika mchezo huu, tungefika mbali sana," alisema Palasa.
Licha ya kuwalaumu wenye dhamana, kiongozi huyo pia alisema hata baadhi ya wadau wa mchezo huo nao ni kikwazo cha kuendelea kwa ngumi kwa vile wanajali zaidi masilahi yao binafsi kuliko masilahi mapana ya mchezo wenyewe.
Palasa (kulia) akiwa katika utambulisho wa pambano kati ya Mfaume Mfaume na Iddi Piarali katika viwanja vya Leaders Club jana. Kulia kwake ni promota wa pambano hilo, Hamis Haruna.
"Kuna wadau wanasumbuliwa na wivu na roho mbaya tu. Wanaona mimi kukalia hiki kiti sifai ila wao ndiyo walistahili. Wanajua ngumi inalipa, lakini badala watoe ushirikiano ili kuukuze mchezo, wanapiga fitina na majungu bila kujua wanaudumaza mchezo wenyewe."

Post a Comment