TUACHENI CHUKI, WASANII WANA CHA KUJIFUNZA KWA DIAMOND
Wakati Michael Jackson akiibuka kuwa kinara wa kundi la familia, The Jacksons Five, miaka ile ya sabini, hakuna hata mwanafamilia mmoja aliyefikiri kuwa mtoto huyo aliyekuwa na umri wa miaka mitano, angekuja kuwa staa wa dunia.
Lakini kipaji ni kipaji. Kadiri miaka ilivyokuwa ikisogea, ndivyo Jacko alivyojitofautisha, si tu na kaka na dada zake wa familia moja, bali na wanamuziki wengine, waupe kwa weusi.
Mwanzo alishambuliwa, akiwemo baba yake mzazi aliyekuwa akimtania kuwa na pua kubwa (hii ndiyo sababu ya yeye kufanya upasuaji wa kurekebisha pua yake) lakini hakujali, aliangalia mbele, kuijua kesho yake na nia yake ya kuiteka dunia.
Alipofikisha umri wa miaka 25, tayari alikuwa untouchable, akiwa na kila kitu ambacho binadamu anatakiwa kuwa nacho katika maisha yake.
Wote tunajua, Jacko Wacko ni nani, hadi anafariki alikuwa ndiye mwanamuziki tajiri kuliko wote waliopata kutokea katika dunia hii. Aliheshimu na kutumia kipaji chake, alijitengenezea nembo yake na akajipa bidii kazini.
Back to my topic.
Leo Tanzania inaye huyu kijana wa Tandale, moja kati ya vitongoji vya uswahilini zaidi jijini Dar es Salaam. Ndiye msanii wa muziki wa kizazi kipya mwenye mafanikio zaidi.
Wakati akianza kujitokeza, nilipata taabu sana kulijua jina lake. Rafiki yangu Said Mdoe ndiye alikuwa kama mtu wake wamawasiliano. Mara kwa mara aliniomba niandike habari za shoo zake, ambazo nyingi alikua akibebwa na Mzee Yusuf, yule Mfalme wa Taarabu, akiwa na kundi lake la Jahazi Modern Taarab.
Aliponiambia dogo anaitwa Diamond, nilitaka kwanza kujua jina lake halisi, Nasib Abdul.
Taratibu akawa anakuja baada ya wimbo wake ule waMbagala, baadae Kamwambie. Alianza kukutana na vikwazo pale kwa Sharobaro Records, akajitoa na kuanzisha Wasafi.
Wengi tulijua ni mbwembwe tu, lakini siku zote muda ni mwalimu mzuri sana. Alipochanua zaidi, akaambiwa si lolote wala chochote kwa Ali Kiba.Hiyo peke yake ilikuwa ni mafanikio maana King Kiba alianza na kujulikana kabla yake.
Nimewahi kukaa na wakongwe wa huu muziki na kupata mawazo yao. Siku moja nilikaa na Mwana FA, nikamuuliza anajisikiaje kuhusu Diamond kuwa na jina kubwa kumzidi.
FA ni legend, akajibu ki-legend. Akasema yeye anajisikia fahari uwepo wa Diamond, kwa sababu watakapomtazama kama Mtanzania, watataka kujua kama kuna wasanii wengine wakali, ndipo watakapomjua yeye na wengine!
The same kwa Q Chillah. Tulikutana Kinondoni makaburini pale, tukimzika Ndanda Cosovo. Huyu, ni mmoja kati ya wasanii ambao Diamond alikuwa akiwapenda na alishawahi kuchaniwa fulana wakati aking'ang'ania kuingia kwenye shoo yake ili na yeye apande.
Chillah, msanii ambaye pia anajua kusakata soka, akapewa taarifa kuwa kuna janki analilia kupanda kwenye jukwaa lake, akaruhusu aingie na akapewa platfom akaimba.
Hapa unamzungumzia Chillah yule, A List Artist. Basi tukawa tunateta, nikamuuliza kama ana mpango wowote wakumuomba dogo colabo.
Akasema Diamond ni msanii mkubwa na yeye ni msanii mkubwa. Kwa vyovyote collabo yao itazaa muziki mkubwa, kwa hiyo hapendi kukurupuka ingawa milango ya yeye kushirikiana na Simba ipo wazi.
Kuna mashabiki na wasanii wanambeza huyu jamaa. Yes ni kawaida, waswahili hatupendani na tunaombeana mabaya always. Lakini when it comes to reality, let us accept.
Diamond ametusua. Amewaacha mbali wenzake kimuziki. Huyu ni mtu ambaye anapaswa kuheshimiwa na wenzake badala ya kupoteza muda wa kumfananisha.
Ofcoz tunao wasanii wengi wazuri, lakini dogo yupo juu yao. Kama tyngeweza, tungejadili namna ya kuwapata akina Diamond wengine wengi badala ya kutaka huyu apotee.
Pale alipofika, ameajiri vijana na watu wazima kupitia Wasafi Media, je vipi tungewapata wengine wenye viwanda, makampuni ya usafirishaji, kilimo na kadhalika?
Tuacheni chuki za kizamani. Pamoja na mapungufu yote ambayo Michael Jackson alikuwa nayo, ikiwemo kuukana uafrika, bado wasanii wote weusi wa Marekani walimchukulia kama alama yao, kila mmoja akitamani kuyafikia mafanikio yake.
Tuwaruhusu vijana washindane, lakini mashabiki tusitake kuwapoteza bali tulenge kuwazalisha wengi zaidi, jambo ambalo linawezekana kabisa.

Post a Comment