NANI BORA KATI YA CHAMA, AZIZ KI NA NTIBANSOKIZA

Mashabiki wa timu mbili kubwa nchini, Simba na Yanga, wana ligi yao binafsi, achana na hii ya NBC Premier League inayoshirikisha timu 16.

Baada ya kuthibitika uwanjani kwamba ubingwa unapokezana majengo ya pale Kariakoo, mashabiki sasa wanatambiana kuhusu ubora wa vikosi vyao, kila mmoja akitamba wao ni bora zaidi.

Leo ningependa nijadili kuhusu mjadala wa ni nani kiungo bora kwa watani, kati ya Stephan Aziz Ki, raia wa Burkina Faso, dhidi ya Mzambia Clatous Chota Chama na Mburundi, Saidoo Ntabanzonkiza.

Kwanza nikiri kuwa Tanzania imepoteza viungo washehereshaji, tokea kupotea kwa kizazi cha Saidi Mwamba Kizota, Hamis Thobias Gaga, Athuman Abdalah China, Issa Athuman, Method Mogella, Ramadhan Lenny, Ally Maumba na wenzao.




Hivi sasa eneo la kiungo, hasa kwa miamba hawa wawili, linatawaliwa zaidi na wageni kwa miaka ya hivi karibuni, ingawa huwezi kuwaondoa mafundi kama Feisal Salum, Sure Boy Abubakar Salum, Jonas Mkude na hata Hassan Dilunga HD.

Aziz Ki anajua, Saidoo anajua na Chama pia anajua. Nani bora kati yao? Kwa shabiki wa soka asiyeegemea Jangwani au Msimbazi, hawa wote ni wachezaji ambao angependa wawemo katika timu yake, lakini kujua aliye bora zaidi, inataka jicho la Tai, yule ndege mwenye uwezo wa kuona windo ardhini akiwa mamia ya maili angani!

Wote watatu ni mafundi wa mipira iliyokufa, wote wanatoa assist, wote wanafunga. Unawatofautisha tu kwa mifumo inayotumiwa na walimu wanaowafundisha.

Chama ni kiungo anayeweza kucheza akiwa eneo lolote la uwanja, kulia, kushoto na katikati. Anaona nafasi ya yeye kutoa pasi kabla hajapata mpira na ndiyo maana anaonekana kama anayefanya anavyotaka pindi akiwa na mpira.

Ni mtulivu akiwa na mpira. Hana papara na mara zote anapenda mpira wa kupasiana. Hachezi rafu, hana hasira uwanjani na si mbinafsi.




Aziz Ki ni kiungo bora lakini akitokea katikati. Hajaweza kuprove kama ana ubora ule akitokea kulia au kushoto. Anapenda mpira wa kasi na ukimuona amepoozesha mpira, ujue ana burudani anataka kuwapa mashabiki.

Fundi hasa wa mipira iliyokufa. Analenga lango lakini kwa mashuti makali. Humuoni akihaha huku nakule uwanjani, lakini muulize Nasiredine Nabi, atakuambia bila Ki, ana maisha magumu uwanjani.

Saidoo, ana sifa kama za wenzake ila yeye anatumia na nguvu pia. Anaweza soka la physic. Akiwa amezungukwa na wachezaji wanaopasiana, hapo ndipo utapenda ubora wake.

Licha ya uzuri huo, Saidoo ana hasira. Hajaweza kukotroo tempa, hasa kama timu yake inatafuta matokeo. Anakuja vizuri kutokea upande wowote wa uwanja, lakini anakua mzuri zaidi akicheza nyuma ya mshambuliaji.

Saidoo hachoki, anapambana mwanzo mwisho, akitumia akili, ufundi na nguvu, ni kama Said Mwamba enzi zake.

Chama na Saidoo wako timu sahihi kwa aina ya mpira wao na utamaduni wa Simba, lakini Aziz Ki anacheza timu ambayo kupasiana sana sio jadi yao.

Miaka yote, tofauti ya klabu hizi mbili ni aina yao ya uchezaji. Kwetu Jangwani kule, tunataka ushindi, pasi tatu tupo golini. Wenzetu wale wamezoea kuremba, kama Wazenji wanavyosemaga, Chenga twawala.

Combination ya Aziz Ki pale Yanga, inamtaka sana Sure Boy, kwa kuwa wote wana kontroo na wanatazama mbele, lakini uwepo wa Khalid Aucho, pamoja na ubora wake, ni kiungo wa kutanua uwanja, utamaduni ambao upo Simba.

Ni kama kiungo punda wa Simba, Muzamir Yasin, ni mzuri, lakini siyo mtu wa soka la maonyesho la Simba, yeye ni mtu kazi, angefaa sana Jangwani


No comments