CCM INA DENI ZAIDI KULIKO WAKATI MWINGINE WOWOTE

Chama Cha Mapinduzi leo kinatimiza umri wa miaka 46, tangu kuzaliwa kwake, alfajiri ile ya Jumapili, Februari 5, 1977 mjini Unguja.

Ni umri wa mtu mzima, ambaye tayari ana watoto walioanzisha miji yao. Kwa zaidi ya miaka sita na ushee, mfumo wetu wa siasa za vyama vingi ulikuwa kama umefifia.

Siasa zile za vyama zilipotea, ikabaki CCM kama chama mama, chama dola. /Uchaguzi uliopita unathibitisha hili.

Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, ameamua kuruhusu urejeo wa siasa za ushindani. Sasa vyama vingine vinarejesha mikutano yake ya hadhara ili kunadi sera zao, kama ilivyokuwa tangu mwaka 1992.

Siasa hizi zinarejea wakati Rais Samia akiwa amefanya vitu vingi vikubwa. Ameendeleza miradi mikubwa ya kimkakati ya mtangulizi wake, John Pombe Magufuli ikiwemo Ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, Ujenzi wa reli ya kisasa SGR, upanuzi wa barabara, bandari na kadhalika.

Rais Samia, mwanamke wa kwanza nchini kukalia kiti hicho, ametoa fedha nyingi, kote nchini kuhakikisha changamoto ya miaka mingi ya watoto wa shule za msingi na sekondari kusongamana madarasani na kukosa viti inaondoka.

Ametoa fedha nyingi katika ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya, mindombinu ya barabara na karibu kila sekta.

Kifupi, Rais Samia kama watoto wa mjini wanavyosema, AMEFUNIKA!

Nimewasikia makada mara kadhaa, wakisema kuwa kitendo cha mama kuupiga mwingi, kutawafanya washindani kutoka vyama vingine kukosa cha kusema na hivyo chama tawala kushinda uchaguzi kirahisi.

Ni kweli Dokta Samia kaupiga mwingi kuliko ilivyodhaniwa, lakini wakati huu chama kikisherehekea utu uzima wake, ni vyema makada wakatambua kuwa kama kuna wakati mgumu kwao waliwaza kuupata, basi ni huu wa sasa.

Tofauti na wanavyodhani kuwa utendaji wa mama utawarahisishia, hali ni kinyume chake. Utendaji wa mama utawagharimu kwa kuwa wanatakiwa kulinda dhamira yake na kutafsiri kwa vitendo mawazo yake.

Ni kweli anatoa fedha nyingi kwa miradi mingi, swali ni je, fedha hizo ziko salama kwa kiwango gani? 

Adui wa CCM zama hizi, si wapinzani wa vyama vingine, bali watendaji wenye uchu, wabinafsi na wabadhilifu walio ndani ya mfumo unaosimamiwana chama tawala.

Badala ya kudhani akina Tundu Lissu watakosa cha kusema, ni vyema kuhakiikisha kwanza wakwamishaji wote wa Ilani ya chama wanawekwa pembeni na wengine kufikishwa mahakamani.

Kama chama kitawadhibiti wachache hawa, itakuwa ni rahisi kuwashinda wapinzani katika sanduku la kura.

Lakini kama mama anatoa mabilioni tuseme ya kuboresha hospitali, shule au soko, halafu wajanja wanajimegea mabilioni hayo kujinufaisha, unasemaje wapinzani watakosa hoja?

CCM wanaweza kumsaidia mama kwa namna hii, badala ya kupiga ramli za wapinzani kukosa hoja.

HAPPY BIRTHDAY CHAMA DUME!

No comments