RAIS SAMIA ABORESHA MIFUKO YA BARABARA NCHINI TANZANIA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameboresha kwa kiwango kikubwa miundombinu ya barabara kote nchini kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 440 kila mwaka ili kukarabati, kuboresha na hata kujenga njia mpya.
Hayo yamesemwa mjini Dodoma jana na Meneja wa Mfuko wa Barabara Tanzania Bara Eliud Nyaulenga wakati wa kikao chake na wajunbe wa kamati mbili kutoka Zanzibar zilizomtembelea ofisini kwake mtaa wa Ammar jijini Dodoma.
Nyaulenga alisema uboreshaji huo wa miundombinu ya barabara umeweza kurahisisha usafiri na usafirishaji miongoni mwa wananchi na kwamba makusanyo ya fedha za ushuru barabarani yamepanda kwa asilimia 27 kuanzia mwaka wa fedha wa 2019/20 ya shilingi bilioni 806.7 hadi 2021/22 kiasi cha bilioni 1,027.
Nyaulenga ambaye pia ni Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha Mifuko ya Matengenezo ya Barabara Afrika kanda ya Afrika Mashariki, alitaja chanzo kikuu cha mapato ya mfuko huo ni ushuru wa mafuta unaotokana na sheria ya ushuru wa barabara na mafuta sura 220.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kuandaa Mwongozo wa Utumiaji Barabara Zanzibar CPA Bakari Rashid na Omary Makame ambaye nivMwenyekiti wa Kamati ya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mfuko wa Barabara Zanzibar, walieleza kufurahishwa kwao na kile wanachojifunza kutoka Mfuko wa Barabara Tanzania Bara.
Walisema wametembelea barabara zote za Unguja na Pemba na kujionea hali halisi, hivyo katika ziara yao ya siku mbili katika mfuko wa barabara Tanzania Bara wana mengi ya kujifunza.
Hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Rais Hussein Mwinyi, aliunda Mfuko wa Barabara Zanzibar ili kuimarisha barabara za visiwani.
Imetolewa na Mfuko wa Barabara

Post a Comment