DIAMOND ANAJUA KINACHOENDELEA WASAFI PRESENTER SEARCH,?
Niwe muwazi. Mimi ni mvivu sana wa kuangalia vipindi vya televisheni, mara nyingi hutazama tu taarifa za habari. Hata taarifa hizo zinatofautiana kati ya kituo na kituo, huhakikisha nimetazama zote. Tatizo moja kubwa la vituo vyetu vya televisheni, vimekariri kuwa saa mbili usiku ndiyo muda sahihi wa kurusha taarifa hizo za habari.
Ukiondoa taarifa za habari, hupenda pia kutazama habari za michezo na chambuzi zake, ingawa katika eneo hili hutegemea ni habari au mada gani inajadiliwa na zaidi uelewa wa wachambuzi wenyewe.
Mana kusema ukweli, siku hizi kila mtu ni mchambuzi. Hii imepelekea baadhi ya vituo kulazimisha vipindi vya michezo ili mradi kuwepo na uchambuzi. Kwa maoni yangu, jambo hili linafifisha uwezo wa wachambuzi halisi, wenye vipaji, uelewa na mapenzi kwenye michezo yenyewe ambao nchi tumejaaliwa kuwa nao.
Sasa jana katika kutafuta nini naweza kutazama kwa muda niliokuwa nao, majira ya usiku nikakutana na kipindi cha kutafuta vipaji vya watangazaji. katika kituo cha televisheni cha Wasafi, kilichopewa jina la Wasafi Presenter Search.
Nikakipenda kipindi hicho, maana wazo lake ni jema sana. Katika moja ya vitu ambavyo huwa sivutiwi navyo, ni utaratibu usiopendeza wa taasisi na mamlaka zetu za ajira kuthamini zaidi vyeti badala ya vipaji.
Hii ndiyo sababu kubwa inayotufanya tunakuwa na watu wasio sahihi kwa sababu tu walikuja na vyeti, bila kujali walivipataje huko walikotoka.
Lakini bahati mbaya, nilikichukia kipindi hicho ndani ya dakika moja au mbili tu za kukitazama.
Washiriki, ambao ni vijana waliitikia wito kwa wingi sana na wanaonekana waliiandaa sana, Waandaaji wa wazo hilo moja kati ya makosa yao makubwa ni muda na waendeshaji wa shindano.
Haya ni maeneo ambayo walifeli sana. Ninamfahamu Nasibu Abdul, nimemuona akikua, kiumri na kisanii na kimafanikio pia. Kabla hajawa Diamond Platnum huyu tunayemfahamu, amepitia madhira mengi.
Sina uhakika nani aliasisi wazo hilo zuri pale Wasafi, lakini nina uhakika historia ya Diamond kimuziki ilizingatiwa. Kuna nyakati alikuwa akitukanwa akipanda jukwaani, alizuiwa kuingia kwenye shoo za wenzake na hata alilazimika kutoa hela ili aandikwe magazetini.
Wote waliomzuia kusogea, hawakujua kipaji chake na hawakufikiri kuwa wanamchelewesha mtu ambaye atawainua vijana wenzake wengi kwa kadiri atakavyoweza.
Ile ajira anayotoa kwa vijana wenzake pale Wasafi Media ni matunda ya uvumilivu wake.
Katika Wasafi Presenter Search, nimeziona dosari mbili ambazo kwangu zinakwaza wazo zuri mno. Kwanza muda..
Niliona waendeshaji wanauliza mshiriki kaja na nini, jambo ambalo ni zuri kwa sababu si kila mtu anataka kutangaza kila jambo. Kwa hiyo mtu anajiandaa kwenda kuonyesha uwezo wake katika vipindi labda michezo, muziki, taarifa ya habari, uchambuzi wa michezo na kadhalika.
Halafu anapewa sekunde 30 kuonyesha hicho alichonacho!!!Huu ni utani. Hivi kuna mtu anaweza kuonyesha uwezo wake ndani ya sekunde 30?
Lazima tutambue kuwa wale washiriki bado vijana wadogo kiasi hata ule uwezo wa kujiamini pia ni mdogo. Sekunde 30 ni chache sana kwa si tu mshiriki kuonyesha uwezo wake, bali hata huyo mgundua vipaji hana uwezo huo!
Utatambua kipaji cha mtu kwa kumtazama au kumsikiliza mara kadhaa au angalau kwa muda fulani,
Jambo ambalo waandaaji wanapaswa kujua ni kuwa zoezi hilo linafanyika live, watu wana kihoro, wanahitaji kujibalansi ili kurudisha komfidensi yao taratibu.
Ushauri wangu kwenye eneo hili, waandaaji waongeze muda wa washiriki kubaki kwa stage. Angalau dakikà tatu au kumuacha mtu amalize alichoandaa. Najua muda ni mchache, lakini huwezi kupata kilicho bora kwa haraka!
Dakika moja inaweza kumtoa hofu na dakika mbili ukaona kilicho ndani yake.
Eneo lingine ambalo waandaaji, kwa maoni yangu walibugi sana, ni uchaguzi wa watu wa kuindesha programu ile.
Sisemi moja kwa moja kuwa hawafai, kwa sababu wanaweza kupewa maelekezo na wakafanya vizuri. Hawana lugha inayostahili kwa suala kama lile.
Wale washiriki vijana wanahangaika kutafuta ajira, hujui nini kimetokea hadi akafika hapo studio na isitoshe ndugu, jamaa na marafiki wanafuatilia kwenye televisheni. Moja kati ya vitu muhimu sana kwao, ni lugha rafiki, yenye matumaini na kumtia moyo.
Lakini anafika pale anaanza hata sentensi moja hajamaliza, mtu anamwambia "Inatosha, utangazaji siyo kazi yako, katafute cha kufanya!!!!!!!
Sasa, mmewakusanya wale vijana pale kuwadhalilisha? Kwani kwa mfano, pamoja na kumkatisha kabla hajamaliza sentensi, halafu angeambiwa kwa mfano..."Komredi, hongera sana kwa kujaribu, una kitu ndani yako, hebu nenda kajifue zaidi!!!
Wale waongozaji wana lugha chafu, ya majivuno. Kuna wengine tunawajua, hawana hata miaka mitano ya utangazaji wao, lakini leo wameota mapembe.
Wanasema eti, huwezi kuja kutangaza media kubwa kama Wasafi, nenda kaanzie redio za miikoani ujifue. Hivi Wasafi ni wakubwa?
Anyway, sitaki kujadili jambo hilo kwa leo, ila wale watoto waendesha kile kipindi ama waondolewe ama waelekezwe cha kusema maana huenda wenyewe hawajielewi!

Post a Comment