KATIBU MKUU MALONGO ATOA NENO ZITO KWA TEMESA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Mhandisi Joseph Malongo, akisukuma moja ya kiti cha kusaidia watu wenye uhitaji maalum ,alivyovizindua katika karakana ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mkoani Dodoma. Viti 33 vya watu wenye uhitaji maalum vimezinduliwa na vinatarajiwa kusambazwa katika vivuko vyote nchini.. Picha na WUU
KATIBU MKUU wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Malongo, ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), kuhakikisha unaboresha huduma zake na kuongeza ufanisi kwa watumishi wake ili kuvutia wateja wao ambao wamekuwa wakilalamika kuhusu utoaji wa huduma zao.
Akizungumza katika uzinduzi wa karakana sita zinazohamishika
(Mobile Workshop), vifaa stahiki vya kuchunguza
ubovu wa magari pamoja na viti 33 vya wenye mahitaji maalum kwa ajili ya kusaidia
abiria wanaovuka katika vivuko vyote nchini vinavyosimamiwa na Wakala huo.
Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa licha ya Wakala huo
kuwa na Karakana kila Mkoa, lakini bado huduma zinazotolewa ndani ya karakana hizo
haziridhishi hali inayopelekea washitiri kuamini kuwa Wakala umebweteka kutokana
na kukosekana kwa ushindani wa kibiashara na kuwa ni Taasisi ya Serikali pekee kwenye
matengenezo ya magari.
“Nilivyoingia Wizarani mwezi wa tatu, niliamua kufanya
utafiti kwa baadhi ya Taasisi za Serikali kuhusu utendaji wa TEMESA, nilifanya hivyo
kwa sababu nilikuwa mlalamikaji kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala huu, na matokeo
niliyopata kutokana na utafiti wangu ni kuwa, asilimia 75 yaniliowahoji walisema
kuwa TEMESA wamebweteka na pia wafanyakazi wao kutokuendana na mabadiliko ya teknolojia”,
amesema Mhandisi Malongo.
Ameongeza kuwa utafiti ulibaini kuwa Wakala huo umetawaliwa
na ukiritimba, ukosefu wa uweledi kwenye kazi na ubadhirifu wa vipuri ambapo baadhi
ya vifaa vinavyofungwa katika magari si halisi na huharibika muda mfupi mara tu
baada ya kupatiwa huduma.
Aidha, ameusisitiza Wakala huo kuhakikisha wanaboresha
mkakati wao wa kibiashara na kuboresha usimamizi wa kifedha ambao utalenga kutoa
huduma nzuri kwa wateja wao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi wa Wakala huo,
Profesa Idrissa Mshoro, ameiomba Serikali
kupitia Wakala huo kuendelea kuajiri mafundi wa kutosha ili kuongeza idadi ya mafundi
na kuwapatia ujuzi utakaoendana na mabadiliko ya teknolojia ambayo yatawasaidia
kufanyakazi zao kwa ufanisi.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Maselle,
amesema kuwa, ununuzi wa karakana zinazohamishika umelenga kusogeza huduma kwa wateja
walio mbali na karakana za mikoa na pia kutoa huduma ya matengenezo ya dharura yanayotokea
maeneo yasiyo na karakana hasa magari na mitambo yanapokuwa safarini au kazini nje
ya ofisi.
Ameongeza kuwa viti vya wenye mahitaji maalum vitakuwa
msaada kwa abiria wenye ulemavu ambapo awali huduma hii ilikuwa haitolewi kwenye
vivuko vya Serikali na kusababisha usumbufu kwa abiria wenye mahitaji maalum.
Kuhusu vifaa vya kuchunguza ubovu wa hitilafu za magari
na mitambo, Mhandisi Maselle, amesema kuwa Wakala umepanga kupeleka vifaa hivyo
katika kila kituo na kufafanua kuwa vifaa hivyo vitasaidia kubaini tatizo kwa usahihi
na kwa muda mfupi, kutaboresha huduma na kupunguza muda wa matengenezo ya magari
na mitambo pamoja na kupunguza malalamiko ya wateja kufungiwa vipuri visivyo halisi.
Zaidi ya shilingi Milioni 765 zimetumika katika ununuzi
wa karakana sita zinazohamishika ambazo zitagawiwa katika
mikoa ya Arusha, Mwanza, Mtwara, Mbeya, Tabora na Dodoma, ununuzi wa vifaa 30
vya kuchunguza ubovu na hitilafu za magari na mitambo pamoja na viti 33 vya wenye
mahitaji maalum.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment