USHIRIKINA NI SEHEMU YA MAISHA YA WASWAHILI

MAISHA yana sarakasi nyingi sana. Zipo simulizi za kila aina zinazosimulia jinsi baadhi yetu tunavyoishi katika dunia ya giza. Kuna watu wanakimbia makwao kule vijijini wakiogopa uchawi na wapo ambao hawataki kabisa kurudi huko wakiogopa ushirikina.
Utafikiri labda
huku mijini wanakoishi hakuna wachawi au na wao hawajishughulishi nao. Mijini
ndipo kwenye waganga wengi zaidi, na waswahili wanapishana kwenye milango yao
wakitaka huduma.
Huyu anataka dawa
ya kinga, akidai majirani wanamuonea kijicho, huyu atasema anataka kumfunga
mume wa mtu maana mkewe anambana sana, yule atataka dawa ya kuwa karibu na bosi
ofisini kwake, mwingine atataka afanyiwe mpango amng'oe kitini mwenzake.
Mtu atafungua
kajibiashara kake labda cha kupika maandazi, chapati au kuchoma mihogo, lakini
lazima aende kwanza kwa babu, apewe vimitimiti avitafune ndipo aridhike kwamba
sasa anaweza kuendelea na shughuli. Kwa nini, ana hofu kwamba kwa kuwa watu
hatutakiani mema, basi lazima tu kuna mtu atamtia nuksi.
Hatuna ushahidi,
lakini namna tunavyoendesha maisha yetu, ni dhahiri kuwa mtu anaweza kwenda
'kumshughulikia' mwenzake kwa mganga ili mradi tu amkwamishe mishe mishe zake.
Tena huyo aweza kuwa mtu wake wa karibu kabisa, kila siku akimpelekea shida
zake. Lakini anataka amkwamishe maana anamuona kama anajidai.
Badala
ukamshughulikie ili Mungu azidi kumbariki apate kukusaidia zaidi, eti unataka
na yeye akwame, sasa shida zako utazimalizia wapi?
Watu wanaishi
wanakuambia wanamuomba Mungu tu, ndiye kimbilio lao. Waongo wakubwa...kama kuna
watu wanaojidanganya wenyewe, basi ni wale wanatudanganya kwa kukaa sana kwenye
nyumba za ibada na kushiriki kila sala. Iwe waislamu au wakristo. Kwa utafiti
wangu, hawa ndiyo wanaongoza kwa kumiliki hirizi na kufanya makafara majumbani
mwao.
Unamuona mtu swala
tano kwa ndugu zangu waislamu, lakini kila siku anafanya matambiko nyumbani
kwake, kila siku yupo kwa mtabiri na mganga wa vitabu. Basi bora hayo anafanya
kwa kificho, lakini swala tano huyu kila akikaa sehemu, kazi yake ni kusengenya
wenzake, huyu ana hivi, huyu ana vile. Mcha Mungu gani wewe?
Njoo kwa ndugu
zangu wakristo. Hakosi ibada, iwe wa Jumuia, Jumapili au Hija. Muda wote
utamuona na bibilia yake mkononi, rozari shingoni na sebuleni kwake mabango ya
Yesu yamesheheni. Lakini nyuma ya pazia, ana hirizi.
Ni kweli anamuamini
Mungu, lakini anawaogopa wanadamu. Anajikinga, maana wanasema jisaidie ili
usaidiwe.
Mtu haanzi kujenga
nyumba yake bila kumwaga ungaunga au kufanya kisomo kinachoambatana na
uchinjaji wa kuku au mbuzi. Mtu akipita nyumbani kwake mara mbili au tatu
ameshaanza kumtilia shaka, siyo kwamba ni mwizi, la. Mama au baba mtu mzima
ataiba nini hapa, huyu kuna kitu anataka kufanya!
Maisha yetu
yametawaliwa sana na imani hizi. Hata wenzetu waliofanikiwa kimaisha, bado
hatuwaamini, tunaona kama kuna giza nyuma ya utajiri wao. Utawasikia tu
wanasema, yule mganga wake namjua, aliuaga ndugu zake!
Jamani, kwani mtu
ukifanikiwa ndiyo ndugu zako wasife na wakifa eti umewaua wewe? Hebu huyo
anayesema aliyefanikiwa ameua ndugu zake, je yeye hana ndugu aliyekufa?
Kitu cha msingi na
ambacho ningependa nikuache nacho. Ni juu yako kuamua, uufuate ushirikina au
uuache. Vyovyote utakavyoamua, huna lolote utakalobadili kama hautafanya
jitihada za kutimiza lile ulilolipanga kwa kufuata kanuni zilizopo maana maisha
yetu yote yametawaliwa na kanuni.

Post a Comment