MELI ILIYOZIBA MFEREJI WA SUEZ YAINGIZA HASARA YA MAMILIONI KILA SIKU

 4bxz0ff283dc5b1ud2a_800C450.jpg


 

Inakadiriwa kuwa kuna hasara ya dola milioni nne kwa saa baada ya meli kubwa ya kontena kuziba Mfereji wa Maji wa Suez nchini Misri. Mfereji huo ni kati ya njia zenye shughuli nyingi zaidi za meli za kibiashara duniani.

Kwa mujibu wa makadirio ya Shirika la Lloyd List, baada ya meli hiyo kuziba Mfereji wa Suez, meli zilizokwama kuelekea upande wa maghairbi zinapata hasara ya dola bilioni 5.1 kwa siku na zile zilizokwama upande uneoelekea mashariki zinapata hasara ya takribani dola bilioni 4.5 kwa siku.

Kwa mujibu wa data zilizokusanywa na Shirika la Habari la Bloomberg, hivi sasa kuna jumla ya meli 185 ambazo zinasubiri kupita Mfereji wa Suez. Miongoni mwa meli hizo kuna meli 27 kubwa za mafuta ambazo zina takribani mapipa milioni 1.9 ya mafuta ghafi ya petroli.

Meli iliyoziba Mfereji wa Suez ina urefu wa mita 400 sawa na viwanja vinne vya mpira wa miguu na imekwama kwenye mfereji wa Suez unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari ya Sham na hivyo kuzuia meli kupita huku shughuli mbalimbali muhimu zikivurugwa. Kukwama kwa meli hiyo kumesababisha bei ya mafuta kupanda kwenye masoko ya kimataifa.

Karibu asilimia 12 ya biashara ulimwenguni hupita katika mfereji wa Suez na ni njia ya mkato kati ya Bara la Asia na Ulaya. Meli hiyo iliyosajiliwa nchini Panama na kuendeshwa na kampuni ya usafirishaji ya Evergreen, ilikuwa ikielekea bandari ya Rotterdam nchini Uholanzi ikitokea China na ilikuwa ikipita Kaskazini kupitia mfereji huo kuelekea Mediterranean. Meli hiyo ya tani 200,000 ilitengenezwa mwaka 2018.

Juhudi za kuikwamua meli hiyo zingali zinaendelea huku wakuu wa Misri wakisema huenda zoezi hilo likachukua siku kadhaa.

Meli ambazo haziwezi kusubiri zitalazimika kuzunguka bara Afrika ili kufika Ulaya na hivyo kurefusha safari kwa takribani wiki mbili zaidi.

No comments