Lushoto DC yapokea mbegu ya Ngano toka ASA
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Mhe. Mathew Mbaruku pamoja na Mkurugenzi Mtendaji (W), Ndg. Ikupa H. Mwasyoge leo wamepokea mbegu ya ngano aina ya safi kutoka kwenye Shamba la Mbegu la Arusha ASA.
Mbegu hiyo ambayo inatarajiwa kugawiwa bure kwa Wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, imetolewa na shamba la mbegu la ASA la Arusha ni mwendelezo wa harakati za uongozi wa Halmashauri wa kuwahamasisha wakulima kupanda zao hilo muhimu la kibiashara.
Akizungumza baada ya kupokea mbegu hiyo, Mhe. Mbaruku, alisema kwamba mwaka jana Halmashauri iligawa mbegu tani 19 kwa wakulima ambayo ilizalisha zaidi ya tani 300 kitu ambacho ni ushahidi tosha kuwa zao hilo linastawi sana Lushoto, ndiyo maana safari hii wameomba zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto alisema kwamba kwa kutumia wataalam wa Halmashauri ofisi yake itahakikisha zao hilo linakuwa na tija kwa wakulima huku akiipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki kwa wakulima na wafanyabiashara kufanya shughuli zao.
Naye Kaimu Afisa Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Ngd. George Madeye, alisema kwamba kutokana na uwepo wa uhitaji mkubwa wa ngano kwenye soko la dunia ndiyo maana wameona kuna umuhimu wa kuwashauri wakulima kulima zao hilo la kibiashara ili kuboresha vipato vyao.
Madeye aliongeza kusema kwamba wataalam wa kilimo (maafisa ugani) waliopo kwenye kata na vijiji watashirikiana na wakulima kutoa ushauri wa kitaalam kuanzia hatua ya kuandaa shamba, kulima, palizi na mavuno ili kuongeza uzalishaji.
Kwa upande wake Mwakilishi wa ASA, Ndg. Abdon Kaijage Juvenul aliwashauri wakulima kutumia mbegu hii aina ya safi kwa sababu ina mavuno makubwa sana ambapo katika hekari moja mkulima anaweza kuvuna zaidi ya gunia 60 kama atalima kwa kuzingatia njia sahihi za kilimo.

Post a Comment