Jukwaa la wazalendo huru Tanzania lachangia milioni moja maafa Hanang
Taasisi ya Jukwaa huru Tanzania imechangia shilingi milioni moja kusaidia jitihada za serikali katika kusaidia waathirika wa maporomoko ma mafuriko huko Hanang mkoani Manyara.
Naibu Afisa Habari wa Jukwaa hilo, Madam Mariam Msede, ameiambia Ojuku Blog kwamba wao kama ilivyo kwa watanzania wote, waliguswa na maafa hayo, hivyo wakaona ni vyema kusaidiana na serikali katika kuwafariji waathirika kwa kutoa mchango wao.
"Sisi kama Watanzania tunatambua jitihada kubwa zinazofanywa na serikali katika kuwasaidia waathirika ili warejee katika maaisha yao ya kawaida. Na kama ambavyo taasisi nyingi na watu binafsi walivyojitolea kusaidia, nasi tukaona tutoe chochote" alisema Madam Mariam.
Alisema Taasisi hiyo inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Mohamed Mwampogwa, Mwenyekiti Yahaya Calamva na Katibu Mkuu Catherine Mapunda, hivi sasa wanajichanga ili waweze kusaidia waathirika wa mafuriko yaliyotokea Kilosa mkoani Morogoro.
"Tunajichanga tena ili tuweze kutoa chochote kwa watanzania wenzetu waliopatwa na mafuriko huko Kilosa mkoani Morogoro. Nitumie fursa hii kuwaomba watu binafsi wenye uwezo, wafanyabiashara, kampuni na mashirika mbalimbali, kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kwa dhati kuwasaidia waathirika wa majanga haya," alisema.
Majanga ya maporomoko ya milima na mafuriko huko Hanang yalipoteza maisha ya watu zaidi ya 80, huku nyumba za wakazi na miundombinu mbalimbali ikiharibiwa.
Kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni, serikali inaendelea na juhudi za kurejesha miundombinu iliyoharibiwa na hadi sasa imefanikiwa kwa karibu asilimia 75.

Post a Comment