Vita vya Gaza: Mtaalamu wa haki kutoka Umoja wa Mataifa aishutumu Israel kwa vitendo vya mauaji ya kimbari
Mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa anasema anaamini Israel imefanya "vitendo vya mauaji ya kimbari" huko Gaza.
Francesca Albanese, ripota maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, aliwasilisha ripoti yake kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva siku ya Jumanne.
Lakini Israel tayari imetupilia mbali matokeo yake.
Haya yanajiri huku kukiwa na shinikizo la kimataifa kwa Israel kusitisha vita au kufanya mengi zaidi kuwalinda raia.
Bi Albanese alihitimisha kuwa "kuna sababu za kuridhisha za kuamini kwamba kiwango kinachoonyesha kutendeka kwa uhalifu wa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina kama kundi huko Gaza kimefikiwa".
Kabla ya Bi Albanese hata kusimama, matokeo yake yalitupiliwa mbali na Israel, ambayo balozi wake alieleza kuwa ni "upotoshaji wa kutisha wa Mkataba wa Mauaji ya Kimbari".
Israel kwa miaka mingi imekuwa ikikasirishwa na ajenda ya Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, ambalo linatoa sehemu nzima - Kipengee cha 7 - kuchunguza hali ya "Palestina na maeneo mengine ya Kiarabu yanayokaliwa".
Kipengele cha ajenda kiliidhinishwa sio na UN yenyewe, lakini na nchi wanachama wa UN miongo kadhaa iliyopita, na haijawahi kuisha. Hakuna nchi nyingine duniani ambayo ina uchunguzi wa kudumu kama huu, na Israeli inaiona kama ya kibaguzi, na inayolenga kuiondoa Israeli. Inakataa kuhudhuria baraza wakati Kipengee cha 7 kinajadiliwa.
bbc

Post a Comment